January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biashara United wawatisha Prisons

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mara

KIKOSI cha timu ya Biashara United leo kitakuwa katika Uwanja wake wa nyumbani wa Kumbukumbu ya Karume, Musoma kusaka alama tatu muhimu katika mchezo wao namba 147 wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Maafande wa Tanzania Prisons.

Timu hiyo itaingia tena katika uwanja wao wa nyumbani kusaka alama tatu nyingine muhimu baada ya kupata ushindi wa goli 3-0 katika mchezo wao uliopita dhidi ya timu ya Mbeya City uliowaweka katika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi baada ya kufikisha pointi 23.

Timu hiyo ambayo imeshinda mechi sita, mechi tano imeshinda katika uwanja huo wa Karume na kushinda mechi moja ugenini jambo linalowapa matumaini kuwa alama tatu za dhidi ya Prisons zitasalia katika uwanja huo.

Kocha wa timu hiyo, Francis Baraza amesema kuwa, mchezo huo ni muhimu sana kwao kwani alama tatu wanazozisaka zitazidi kuwaweka kwenye nafasi bora zaidi katika msimamo wa Ligi.

Amesema kuwa, licha ya kutambua kuwa watakutana na mchezo wa ushindani lakini kiu waliyonayo vijana wake ya kutaka kuendeleza ushindi katika uwanja wao wa nyumbani anaamini itawarahishia kazi.

Kocha huyo amesema, pia wanahitaji kwa hali na mali ushindi kwani katika wanahitaji kumaliza mzunguko wa kwanza kwa ushindi na kuwapa mashabiki wao furaha na kuanza hesabu za mzunguko wa pili.

“Mchezo wetu wa leo ni muhimu sana kwetu na ninaamini kuwa alama tatu zitabaki nyumbani ili kuendeleza furaha ya mashabiki wetu lakini pia kuweka hesabu sawa kuelekea mzunguko wa lala salama hivyo nawaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuja kutupa sapoti,” amesema kocha Baraza.