December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki,taasisi za fedha zatakiwa kupunguza riba

 Na Penina Malundo

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameitaka benki na taasisi mbalimbali za fedha nchini  kupunguza riba na gharama za mikopo, ili kutoa fursa kwa wanawake wajasiriamali kukopa na kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam Jana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mpogolo katika Jukwaa la Utayari na fursa lililoandaliwa na Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kupitia mradi wake wa Employment and Skills for the Development in Afrika (E4D).

Amesema ni muhimu benki kuwa na mikopo rafiki riba nafuu kwa wanawake kwa sababu ndio watu wenye uhakika wa kurejersha fedha hizo kuliko wanaume ambao mara nyingi wamekuwa ni shida.

“Niwasihi benki mbalimbali kupunguza riba ili iweze kuendana na kasi ya kina mama wanayokwenda nayo, kutokana na riba kuwa juu ndio maana wanawake wanapata shida na kukimbilia mikopo ya halmashauri ya asilimia 10 ambayo peke yake haiwezi kuwatosha,” amesema.

Aidha amesema kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo wanawake wanazipitia katika masuala ya fursa, mitaji na masoko ambazo zinapaswa kutatuliwa ili kuliwezesha kundi hilo kufanya biashara kwa uhuru na kujiingizia kipato.

“Moja ya suluhisho la jambo hilo ni kutumia masoko mtandao, hii ni fursa ambayo ikitumiwa vizuri itawakomboa wanawake wengi kiuchumi, leo hii mjasiriamali unayefikiria kutengeneza batiki na umepanga kutumia milioni 10 tenga kiasi kingine kwa ajili ya soko mtandao ambalo ukilitumia vizuri itakusaidia kujitangaza na kuuza bidhaa zako,” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TWCC, Mercy Sila aliwataka wanawake kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuweza kuingia katika masoko makubwa ya kimataifa ya biashara na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Sila amesema kwa sasa fursa za kiuchumi ni nyingi na Serikali imekwisha weka mazingira wezeshi ya wanawake kujikwamua hivyo ni muhimu kwa kundi hilo kuungana kwa pamoja na kufanyakazi kwa ushirikiano.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza amesema kazi yao ni kuhakikisha kwamba wanawake wanapata fursa za kiuchumi, wanashiriki kuzalisha ajira, kukuza kipato na kuchangia pato la taifa

Aidha Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ-E4D), Kabongo Mbuyi amesema wameamua kufadhili jukwaa hilo na kushirikiana na TWCC kwa lengo la kuwawezesha wanawake wajasiriamali kujikwamua kiuchumi.

“Tumekuwa tukifadhili program mbalimbali za wanawake lakini tumevutiwa na TWCC kwa kuwa wanafanya kazi kubwa ya kuwainua wanawake lengo likiwa wajikwamue kichumi na kukuza pato la taifa la Tanzania,” amesema.