January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yatenga Bil 5/- kwa mikopo ya Bodaboda

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amewataka madereva wa pikipiki za abiria maarufu kama ‘Bodaboda’ kujiwekea hesima ili watambulike katika ajira rasmi na kukopesheka.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akizindua mfumo wa kukopesha pikipiki kutoka Benki ya NMB, NMB MASTABODA – MILIKI CHOMBO uliofanyika ukumbi wa Ubungo Plaza.

Waziri Mhagama amebainisha kuwa uongozi wa Benki ya NMB umefanya kitu kikubwa kwa kuwakumbuka madereva wa bodaboda kuwa wanawagusa wateja wadogo wenye mahitaji makubwa katika huduma zao.

“Rais Samia Suluhu Hassan, anasema kila mmoja ashiriki katika kukuza uchumi wa nchi kwa kufanya kazi, hivyo nanyi waendesha bodaboda mnao wajibu wa kufanya kazi na kulinda nidhamu na mnafahamiana, wale wakorofi wanaowaharibia sifa zenu mnapokuwa kwenye shughuli zenu,” amesema Mhagama.

“Lindeni heshima yenu ili jamii iwaheshimu na Isiwachukulie kama watu msio na ajira rasmi. Ndio maana ninaziomba taasisi nyingine za kifedha ziige mfano wa Benki ya NMB kuwakumbuka watu wa chini, wawakumbuke waendesha bodaboda nchi nzima muweze kukopesheka nanyi mmiliki pikipiki zenu badala ya kuendelea kuwatumikia watu wengine.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema utekelezaji wa NMB Mastaboda- Miliki Chombo ni matokeo ya agizo alilolitoa Waziri Mhagama mnamo Oktoba, 2019 wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye kampeni ya kulipia nauli ya bodaboda kwa kutumia mfumo wa MasterCard QR iliyoitwa MastaBoda.

“Itakumbukwa Waziri wakati ukizindua utaratibu wa kulipia nauli za bodaboda kwa kutumia mfumo wa QR Card, ulituagiza tuweke utaratibu wa kuwakopesha pikipiki hawa madereva wa Bodaboda. Tulikaa tukajadiliana tukaamua kuja na wazo hili, tunafahamu kuna zaidi ya waendesha Bodaboda milioni mbili nchini lakini hawapo kwenye mfumo rasmi wa kibenki na wengine hawana ajira rasmi. Tunaamini utaratibu huu utawaleta pamoja na watatambulika kama watu wenye ajira rasmi,” amesema Zaipuna.

Aidha amesema, dereva wa Bodaboda atakayekuwa kwenye kikundi na kufuata taratibu za kutambulika kisha akakopeshwa pikipiki na Benki ya NMB, maana yake atakuwa miongoni mwa wateja ambao atamiliki chombo chake, hivyo tayari atakuwa katika ajira rasmi ambapo wapo watakaomiliki pikipiki zaidi ya moja za miguu miwili na mitatu.

“Kwa kuanzia tunaanza na madereva wa Bodaboda wa Dar es Salaam, tumewatengea Shilingi Bilioni 5 mwaka huu. Mwitiko ukiwa mkubwa tutaongeza fedha kwa kadiri ya mahitaji na kuongeza ubunifu zaidi ili kukuza uchumi na kuongeza ajira hasa kwa vijana,” amesema Zaipuna.

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi, Biashara Ndogo na za Kati Benki ya NMB, Filbert Mponzi amesema, utaratibu ulivyo dereva wa Bodaboda atatakiwa kufungua akaunti ya NMB kama hana, kisha atasubiri ndani ya miezi mitatu huku akiendelea kufanya miamala ili kuwa na sifa za kukopesheka.

“Mteja anatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa kuonyesha ni raia lakini pia kuwa na leseni ya udereva mpaka sasa tayari wapo madereva wa Bodaboda 5,000 katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao wamewapa mafunzo ili wapate mkopo lazima upate elimu na namna ya kuutumia na nidhamu ya kutunza fedha,” amesema Mponzi.

Amesisitiza kuwa atakayepata mkopo wa pikipiki ya miguu miwili au mitatu au pikipiki ya mizigo ya miguu mitatu, hapo hapo anakuwa ameshajiunga na mfumo wa bima. Maana yake kama kutatokea dharura yoyote anakuwa na uwezo wa kulipwa chombo kipya.

%%%%%%%%%%%%