Na Esther Macha, Timesmajiraonline, Mbeya
BENKI ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu imetenga sh. Bil.100 kwa ajili ya kusaidia nishati safi kwa ajili ya wajasiriamali katika maeneo mbalimbali lengo likiwa ni jitihada za kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika harakati za kutunza mazingira.
Hayo yamesemwa Mei 10, 2025 na Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu ,Wogofya Mfalamagoha, wakati wa kuhitimishwa kwa mashindano ya Riadha Mbeya Betika Tulia Marathoni ambazo zilihitimishwa katika viwanja vya kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya, ambapo mgeni rasmi katika mbio hizo alikuwa Naibu Waziri Mkuu Dkt.Dotto Biteko.
Aidha Mfalamagoha alisema kuwa wamekuwa wakiwapa nishati hiyo safi wajasiliamali ambao wanasambaza nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ili kuweza kumfikia kila mwananchi ili aweze kutumia nishati safi ambayo lengo lake ni kutunza mazingira.

“Lakini tumekuwa tukienda mbali zaidi katika masuala ya mazingira kama ambavyo Spika alisema kuwa ni ajenda kubwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambayo sisi kama Benki ya NMB tunasapoti ,hivyo ni mkakati mkubwa ambao tumeingia kwa kusapoti sh. bilioni 100 na tunatoa riba wezeshi kuhakikisha kuwa kila Mtanzania atumia nishati safi,”alisema Mfalamagoha.
Akizungumzia kuhusu kusaidia michezo ambayo yanaenda kuboresha afya za Watanzania, Mfalamagoha alisema kuwa pia walisapoti hospitali ya (CCBRT) kwa kuweka Bl.100 ,mbio za mwendo wa upendo ambapo waliweka sh. Bil.100 pia kwa ajili ya kusapoti wanawake wenye changamoto ya Fistula ambao waliweza kupata matibabu na wengine wanaendelea kupata matibabu.
Akielezea zaidi Meneja huyo alisema kuwa kwa upande wa vijana kuna akaunti ambayo inafunguliwa kwa sh. 1000 tu .
Meneja huyo alimpongeza Dkt Tulia kwa ubunifu ambao amekuwa akifanya kwa sababu kila mtu anafurahia pia alipongeza jitihada za Tulia Trust kwa Kazi kubwa waliyofanya.
Mmoja wa washiriki wa mashindano ya Riadha Mbeya Betika Tulia Marathoni ,Zulfa Abdallah, alisema uwepo wa akaunti ya vijana ambayo kiwango chake ni kidogo imekuwa msaada mkubwa kwa vijana wenye kipato cha chini kwani imefanya asilimia kubwa ya vijana kujiunga na akaunti hiyo.
“Lakini uwepo wa Tulia Marathoni ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka umeleta fursa kwa wajasiriamali wadogo kuweza kufanya shughuli zao ndogo ndogo za kuingiza kipato .
Benki ya NMB katika mashindano ya Riadha ya Mbeya Betika Tulia Marathoni ni moja wadhamini wakubwa katika kufanikisha mashindano hayo .
More Stories
Dkt. Biteko avutiwa mwitikio Tulia marathon
Mapato yasiyo ya kodi yafikia asilimia 67, OMH yadhamiria kufikia lengo la mwaka
Watu Wenye Ulemavu wamchangia Samia Milioni 1 kwa ajili ya Fomu ya Urais