November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yapiga jeki Zahanati ya Kijiji cha Ivilikinge Wilyani Makete

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Makete

Benki ya NMB imekabidhi vifaa tiba ikiwemo vitanda na mashuka katika Zahanati ya Kijiji cha Ivilikinge wilyani Makete mkoani Njombe vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni tisa.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo mwishoni mwa wiki, Kaimu Meneja Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Willy Mponzi alisema benki hiyo kila mwaka imekuwa na utamaduni wa kutenga asilimia moja ya pato lake baada ya makato ya kodi kwa lengo la kurudisha kwa jamii.

“Msaada huu ambao leo tumekabidhi Makete pia tumekuwa tunakabidhi katika sehemu mbalimbali katika nchi yetu na huu msaada umehusisha vifaa tiba,” amesema Mponzi.

Alisema awali wakati zahanati hiyo inaanza ujenzi, benki hiyo pia ilichangia bati zenye thamani ya milioni nane.

Aidha alisema kuwa, kwa miaka kadhaa sasa NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye miradi ya elimu ambayo inahusisha madawati, vifaa vya kuezekea lakini kwenye vituo vya afya wametoa vitanda, magodolo na vifaa vyengine vya matibabu.

“Na pia benki ya NMB tumekuwa tukisaidia nchi yetu kwa majanga mbalimbali, tunatambua kuwa ni kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka,” amesema Mponzi.

Naye Katibu wa Chama cha Maendeleo Makete (MDA), Award Mpandila aliishukuru NMB kwa msaada huo na kuwaomba kuendelea kuboresha mahusiano yaliyopo kati ya NMB na wananchi.

Kwa Upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana aliishukuru benki ya NMB kwa kuunga mkono jitihada za serikali na wananchi na kuwataka kuendelea kushirikiana ili kuleta tija kwa taifa.

Awali Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kijiji cha Ivilikinge, Hassan Yusuph alisema mara baada ya wananchi kuibua mradi wa ujenzi zahanati benki ya NMB iliwasaidia bati yenye thamani ya shilingi milioni nane.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda aliiomba benki ya NMB kuwaunga mkono pia kwenye ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa zahanati hiyo.