December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB yaongoza Tuzo za Mwajiri bora wa mwaka 2022

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya NMB imetangazwa kuwa Mwajiri bora wa mwaka 2022 katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma.

Benki hiyo mbali na kushinda Tuzo ya mshindi wa jumla kama Mwajiri Bora wa Mwaka pia ilinyakua tuzo nyingine mbili za Mwajiri mkubwa zaidi na tuzo ya Mwajiri Bora wa Jumla kwenye Sekta Binafsi na kufanya jumla ya tuzo ilizoshinda benki hiyo kufikia 21 hadi sasa mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hizo, Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay alisema kutajwa kuwa mwajiri namba moja nchini kunatambua weledi wa benki hiyo katika kufata misingi bora ya utumishi huku ikiwajengea wafanyakazi wao mazingira wezeshi ya kiutendaji.

“Tunafurahi kwamba leo tumetunukiwa tuzo ya Mwajiri Bora wa ujumla baada ya kushinda tuzo nyingi mwaka huu. Maono yetu ni kuwa taasisi inayoongoza katika kusaidia kujenga mustakabali mwema kwa Watanzania wote. Kama sehemu ya mkakati wetu wa biashara, tunawekeza pakubwa katika kujenga utamaduni jumuishi ambapo wafanyakazi wetu  wanathaminiwa  na kushirikishwa katika mambo yanayohusu biashara na maslahi yao” Akonaay alisema.

Akonaay aliongezea kuwa benki yake inatoa kipaumbele kwa wafanyakazi wake na kutilia mkazo katika kujenga na kuendeleza uwezo wa viongozi sehemu za kazi kama sehemu ya mkakati wake wa kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu nchini kote.

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako alidokeza kuwa Serikali imedhamiria kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta binafsi baada ya kupitisha kima cha chini cha mishahara kwa watumishi wa sekta binafsi ambacho kitaanza kutumika rasmi Januari 1, 2023.

Makamu wa Rais Philip Mpango ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo aliwataka waajiri kuzingatia sheria za kazi za nchi na kuongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wafanyakazi juu ya unyanyasaji kutoka kwa waajiri na kuongeza kuwa wafanyakazi wa kigeni wanapaswa kuajiriwa haswa ambapo ujuzi haupatikani kwa urahisi nchini.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango (kulia) akimkabidhi Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay (katikati), Tuzo ya Mwajiri Bora 2022 baada ya NMB kuibuka mshindi wa jumla katika hafla ya utoaji tuzo hizo zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango (wapili kulia), akimkabidhi Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay (wapili kushoto), Tuzo ya Mwajiri Bora 2022 baada ya NMB kuibuka mshindi wa jumla katika hafla ya utoaji tuzo hizo zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE). Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako na kulia ni mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa ATE, Jayne Nyimbo.