Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
Benki ya NMB imedhihirisha tena ukubwa wake nchini, baada ya mwaka huu kuweka rekodi kwa kutwaa zaidi ya tuzo 30 zinazotambua ubora wa huduma zake, ubunifu, ufanisi katika uendeshaji na utendaji, pamoja na mchango wake mkubwa katika ujenzi wa taifa.
Mafanikio hayo ya kipekee kitasnia na makubwa kitaifa na kimataifa yalibainishwa jana jijini Mwanza na Afisa Mtendaji Mkuu, Bi Ruth Zaipuna, katika mkutano wa viongozi wakuu wa benki hiyo pamoja na mameneja wa matawi yake zaidi ya 240.
Akizungumza pembezoni mwa mkutano huo, Bi Zaipuna alisema ushindi huo ni hatua kubwa kwao inayotokana na juhudi za wafanyazi pamoja na uwekezaji unaofanyika katika teknolojia za kisasa na kubuni masuluhisho ya kuwahudumia wateja na taifa kwa ujumla.
“Mwaka huu tumeshinda zawadi mbalimbali na tuzo zaidi ya 30 za kitaifa na kimataifa zikiwemo zile za Benki Bora Tanzania kwa Mwaka 2024, kutoka jarida la Euromoney; Ubunifu Bora katika Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi kutoka International Banker Magazine; na Benki Bora Huduma Ujumuishi za Kifedha 2024 ya jarida la World Economic Magazine,” alimwambia mgeni rasmi wa mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Bw Ng’wilabuzu Ludigija.
Aidha, alimueleza kiongozi huyo kuwa kwa mara 11 mfululizo katika miaka 12, NMB imekuwa ikitwaa tuzo ya benki bora na kuwa ushahidi wa umahiri wake wa ubunifu ni masuluhisho mpya inayoyatambulisha sokoni kila kukicha na mfano mzuri wa hilo ni huduma ya NMB Jiwekee iliyoanza mwaka huu.
Upande wa ujumuishaji kifedha, Bi Zaipuna alisema kupitia Mkakati wa Benki Vijijini, wanatarajia mwakani kuhakikisha kila kijiji nchini kinafikiwa na huduma za kifedha. Mchakato huu, aliongeza, unachangia pia kufanya sekta isiyo rasmi kuwa sehemu ya uchumi rasmi na kusaidia kupanua wigo wa kodi nchini.
“Pia tunafanya vizuri upande wa usawa wa kijinsia mahala pa kazi na kufadhili jitihada za kuwakwamua kifedha na kuwawezesha kiuchumi akina mama, kwa hiyo tumeshinda pia tuzo kadhaa katika eneo hili,” iliongeza na kusema kwa sasa asimilia 48 ya wafanyakazi wote wa NMB ni wanawake na waliobaki asilimia 52 ni wanaume.
Tuzo ilizoshinda NMB mwaka huu zinahusiana na masuala ya kijinsia ni pamoja na kuibuka Mshindi wa Jumla – Afrika Mashariki: Kiongozi wa Usawa wa Kijinsia. Nyingine ni ile ya Uwezeshaji ya Wanawake Mahala pa Kazi, Tuzo ya Taasisi Inayoongoza Uwekezaji kwa Vijana wa Kike pamoja na Nishani ya Fedha – Mfadhili Mahiri wa Wajasiriamali Wanawake.
Majarida mengine ya kimataifa na taasisi za ndani nan je zilizoitunuku tuzo NMB mwaka huu ni pamoja na Global Banking & Finance Awards® Review, Global Business Magazine, International Business Magazine, Global Brands Magazine, na Shirika la IFC na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE)>
“Mwaka huu tumepokea tuzo zaidi ya 30 za kitaifa na kimataifa na hii ni hatua kubwa sana na tuna kila sababu ya kupongezana kwa hili,” Bi Zaipuna aliwaambia wajumbe wa mkutano huo ambao ufanyika kila mwishini mwaka kutathimini utendaji na kuweka mikakati.
“Nitumie nafasi hii kuwapongeza wafanyakazi wote wa Benki ya NMB kote nchini kwa kufanya kazi kwa uadilifu, bidii, juhudi na maarifa, hali iliyotupelekea kuaminika na taasisi kubwa duniani na kututambua kama benki bora katika maeneo takribani yote.”
Tuzo nyingine ilizozinyakua NMB mwaka huu ni pamoja na ile ya Benki Bora ya Kidijitali, Benki Bora kwa Uwekezaji Tanzania, Benki Bora ya Wateja Binafsi na Biashara, na Tuzo ya Afisa Mtendaji Mkuu Bora kwa Mabenki nchini Tanzania.
Orodha hii inajumuisha pia tuzo za Benki Bora kwa Wateja Wadogo 2024, Mtunza Mali Bora wa Mwaka, Mtoa Hati Fungani Bora, Benki Bora kwa ESG inayohusiana na mambo ya mazingira, jamii na utawala bora, pamoja na tuzo za ubora na ubunifu wa hatifungani ya NMB Jamii Bond.
“Mwaka huu, Benki ya NMB tumeshinda pia tuzo ya Kampuni Bora Iliyoorodheshwa Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa upande wa mabenki,” Bi Zaipuna alisema na kuongeza kuwa kabla ya mwezi Mei walikuwa pia wameshinda tuzo za Benki Bora ya Wateja Maalum na Benki Bora ya Wateja Wenye Mali.
“Pia tumepokea tuzo ya Benki Bora ya Mikopo na Miradi ya Mkakati na Best Trade Finance Bank Tanzania 2024 kutoka kwa International Business Magazine pamoja na Best Trade Partner Bank – Advisory Services 2024 kutoka kwa International Finance Corporation (IFC),” iliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Bw Ludigija, aliipongeza NMB kwa mafanikio makubwa inayoendelea kuyapata na kuchangia katika ujenzi wa taifa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Aliuambia mkutano huo kuwa uwepo wa benki hiyo katika kila eneo nchini kunaifanya kutegemewa na Watanzania karibu wote hata wale wanaoishi vijijini pamoja na viongozi wa ngazi zote kutokana na kushirikiana kwake kwa karibu na Serikali.
Bw Ludigija ameiomba NMB kuendelea kuchangia maendeleo mkoani Mwanza na hususan wilaya ya Kwimba akisema mkoa huo una utajiri mkubwa wa mazao ya kilimo na samaki pamoja na madini.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais