Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
BENKI ya NMB yadhamini Maonesho ya Nane Nane kwa Shilingi Mil. 80/-Kwa kuthamini mchango wa kilimo katika ukuaji wa uchumi nchini, Benki ya NMB imedhamini Maonesho ya Nane Nane kwa kutoa shilingi milioni 80.
Maonesho haya makubwa ya wakulima Nane Nane yanatarajiwa kuzikutanisha zaidi ya nchi 30 na kitaifa yanafanyika Jijini Mbeya kuanzia leo tarehe moja hadi tarehe Nane mwenzi huu.
Akikabidhi mfano wa hundi ya kiasi hicho cha fedha, kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kaimu Meneja wa Kanda Nyanda za Juu – Frank Rutakwa amesema kwa kipindi cha miaka sita cha maonesho hayo ambayo yamekuwa yakifanyika Kitaifa mkoani Mbeya, Benki hiyo imedhamini jumla ya Shilingi Milioni 255.
Aliongeza kuwa, NMB imeweka idara maalumu ya Kilimo na Mameneja Uhusiano kwenye kila Kanda ili kuhakikisha kilimo kinafanikiwa na kinakuwa msingi imara kwa uchumi wa nchi yetu.
Aidha, alisema kuwa ndani ya miaka minne, wamefungua zaidi ya akaunti 644,034 za wakulima nchi nzima.Mwaka huu kwa Mkoa wa Mbeya pekee, wamefanikiwa kufungua akaunti zaidi ya 87,044 za wakulima wa kahawa, mpunga, parachichi, mahindi nk.
Bw. Rutakwa alibainisha kuwa kupitia NMB Foundation, NMB imeweza kutoa elimu ya fedha na mfunzo ya biashara kwa vyama vya ushirika vya wakulima (AMCOS) 1,450 nchi nzima, ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusimamia mapato yao.
Huku kwa Nyanda za juu pekee wameshirikiana na AMCOs zaidi ya 555 zilizopo Mbozi (kahawa), Rukwa (Mahindi, Soya na Ufuta), Chunya (Tobacco), Njombe (Viazi Ulaya).
Akizungumza mara baada ya kupokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 80 kutoka Benki ya NMB, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya-Mhe. Juma Homera aliishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo na kwa kuendelea kuwa karibu na wakulima kwa kuwasaidia pembejeo na Matrekta hivyo kusaidia kukuza sekta ya kilimo nchini.
“Benki ya NMB ni mojawapo ya taasisi za kifedha zinazoongoza nchini kwa kuchangia kwa dhati juhudi za serikali katika kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi na sekta zingine hususani za Elimu na Afya ambazo wamekuwa mstari wa mbele kutoa michango mara kwa mara,” Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi