March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu yateta na wafanyabiashara

Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya

BENKI ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini imekutana na wafanyabiashara wa maeneo mbalimbali jijini Mbeya kwa lengo la kujadili mafanikio na changamoto zinazowakabili, ikiwa ni mwendelezo wa utaratibu wa benki hiyo wa kushirikiana na wateja wake.

Akizungumza Septemba 19, 2025 katika hoteli ya Eden jijini Mbeya, Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha, alisema madhumuni ya kikao hicho ni kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wafanyabiashara na kushirikiana nao katika kutafuta suluhu za changamoto zinazojitokeza.

“Tumekuwa tukipokea maoni kupitia mitandao ya kijamii na kuyafanyia kazi, lakini sasa tumeamua kwenda mbali zaidi kwa kukutana ana kwa ana na wateja wetu. Hata hivyo, wafanyabiashara wasisubiri mpaka changamoto ziwakute ndipo waziseme. Sisi tupo muda wote na mawasiliano yetu yako wazi,” amesema Mfalamagoha.

Aidha, ameshukuru mwakilishi wa wafanyabiashara wa mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na benki na kuhakikisha mikopo inarudishwa kwa uaminifu, jambo linaloendeleza mahusiano mazuri kati ya pande hizo mbili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya NMB, Alex Mgeni, amesema huduma ya NMB Mkononi ambayo awali ilihusu akaunti binafsi, sasa imepanuliwa hadi kwa akaunti za biashara.

“Mfanyabiashara anaweza kuweka fedha kwenye NMB Mkononi na kufanya miamala yake kirahisi.Tunapanga pia kuanzisha huduma ya mikopo kupitia NMB Mkononi ili kuondoa usumbufu wa kwenda kwenye matawi kujaza fomu. Utakopa ukiwa hapo hapo ulipo,” amesema Mgeni.

Naye Erick Chaula, mfanyabiashara kutoka Tunduma, mkoa wa Songwe, amepongeza benki  ya NMB katika utoaji mikopo yake ambayo imekuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi kwa wafanyabiashara walio wengi.

Hata hivyo, ameomba benki hiyo kuboresha kasi ya utoaji mikopo ili kuwafanya wafanyabiashara kuwa na uchumi wenye tija.

“Wakati mwingine mtu unakamilisha taratibu zote lakini mkopo unachelewa sana, hadi miezi minne ndipo upatiwe. Hii inaleta changamoto kwa kuwa mfanyabiashara anakuwa na malengo yake ya haraka. NMB mjitahidi kurekebisha hili,” amesema Chaula.