Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Benki ya KCB imeendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha uchumi kupitia 2jiAjiri Foundation na Shirika la Kijerumani GIZ kwa kuendeleza programu ya kuwajengea uwezo vijana wa kitanzania kwa kuwapatia mafunzo ya ujuzi laini (Soft Skills) kutoka Mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Idara ya fedha kutoka Benki ya KCB, Pascal Machango leo (Julai 27, 2022) wakati akifungua mafunzo kwa wakufunzi kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) ambao wataenda kutoa mafunzo hayo kwa vijana ili kuweza kupata ajira na kujiajiri wenyewe .
Machango alisema kupitia programu hiyo wanatarajia kuwafikia vijana zaidi ya 900 kutoka mikoa mbalimbali yenye lengo la kuwasaidia vijana kwenda kufanya masomo darasani na nje ya darasa kwa vitendo;
“Mwanza tumechukua vijana 200, Morogoro vijana 150, Arusha vijana 150, Moshi vijana 140, Zanzibar 20, Mwanza 300 na vijana hawa watakapomaliza mafunzo yao kuna vijana 230 ambao watatafutiwa ajira moja kwa moja na 230 wengine watapewa mikopo na wengine watapewa vifaa vya kufanyia kazi”
Aidha alisema Sera ya serikali ni kuhakikisha imetoa ajira kwa vijana hivyo serikali lazima ipate wadau ambao wanauwezo wa kutoa msaada kuhakikisha vijana wetu wanaendelea kiuchumi na kufanikiwa Taifa kwa ujumla.
Pia alisema kupitia mafunzo hayo wamewapa kipaumbele wanawake kwa 36% kati ya vijana hao 960 .
Kwa upande wake Meneja Mradi wa programu ya 2jiAjiri Foundation kwa kushirikiana na shirika la kijerumani GIZ, Betty Muruve alisema wanaendelea kutoa kozi mbalimbali kwa kushirikiana na VETA ikiwemo kozi ya Ujuzi, ufundi vyuma n.k katika mikoa mbalimbali ambapo Benki ya KCB ipo;
“Kama Benki ya KCB na GIZ tumeona kwamba tunaweza tukafanya msaada kwa jamii ya kitanzania hivyo tumetamani kuweza kuongeza ujuzi wa vijana wa kitanzania katika sekta ya ujenzi”
Pia Muruve aliwataka vijana wa kitanzania kuchangamkia fursa hizo kwa kuzichukua na kuzifanyia kazi ili kutengeneza maisha yao na maisha ya wale wanaowategemea na kushirikiana nao.
Naye Mwalimu wa chuo Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA), Bahati Mwakatobe aliyasifu mafunzo hayo kwakuwa yataweza kuwasaidia kuwafundisha vijana wengi namna ya kuwalea wawe na ujuzi laini na kupelekea kupata vijana wazuri kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Mwalimu kutoka Chuo cha Elimu na Mafunzo ya ufundi stadi (VETA), Nedvia Matekele alizungumzia namna mafunzo hayo yanavyoleta manufaa katika jamii na soko la ajira kwa vijana;
“Vijana wengi wanakosa ujuzi au maarifa ya kuweza kujiajiri au kuajiriwa hivyo programu hii ya KCB itakuwa ni daraja kubwa sana kwaajili ya vijana wengi ambao watapata fursa na ujuzi ambao unaweza akiwasaidia kwa kuajiriwa au kujiajiri wao wenyewe”Alisema Matekele na kuongeza kuwa;
“Programu hiyo Ni daraja zuri kwa vijana waliowengi ambao uwezo wao wa kiuchumi ni mdogo ambapo KCB itakua ni mkombozi wao ili kwamba waweze kupata ujuzi wa kujiajiri ama kuajiriwa.”
Mradi wa kuwaongezea ujuzi vijana umeanza Septemba 10, 2021 na mpaka kufikia Juni, 2023 wanatarajia kufikia malengo yao.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
CRDB yazindua matawi Majimoto, Ilula kuwahudumia wananchi
Lina PG Tour yafufua gofu Moshi