Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar
BENKI ya Exim Tanzania imefanya tamasha linalojulikana kama‘Exim Bima Festival 2024’, lenye lengo la kuchangangia huduma za afya hususani kwa watu wenye tatizo la afya ya akili.
Katika taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim Tanzania,Jaffari Matundu amesema kuwa katika kusherehekea miaka 27 ya kuwahudumia Watanzania tangu kuanzishwa kwake, benki ya Exim imekuja na ‘Exim Bima Festival 2024’, ikiwa na kaulimbiu ‘Amsha Matumaini’, huku ikiwaleta pamoja wadau kama makampuni ya bima, wafanyakazi, watalaamu wa afya, na wanamichezo katika Viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.
“Tamasha hili sio la burudani tu, ni wito kwa kila Mtanzania kuchukua hatua kuongeza uelewa na msaada kwa watu wenye tatizo la afya ya akili Wakati changamoto za afya ya akili zikiongezeka nchini, tamasha hili ni fursa ya kipee kwa watu binafsi, wadau, taasisi, na sekta mbambali kuungana katika kukusanya fedha kwa lengo la kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wale wanaoathirika na tatizo la afya ya akili,”amesema Matundu.
Ameeleza kuwa Exim Bima Festival 2024 ni moja ya malengo ya mpango wa ‘Exim Cares’ wa Exim Bank Tanzania, tamasha la mwaka huu limepanga kuelekeza nguvu zake katika kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika jamii yetu huku likijikita katika kusaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za afya ya akili na ustawi wa jamii ya Watanzania kote nchini.
Matundu amesema Benki ya Exim imejiwekea lengo la kukusanya jumla ya TZS milioni 300 ndani ya miaka mitatu ijayo ili kugharamia huduma muhimu na maboresho ya miundombinu katika vituo vya afya ya akili.
“Siku ya leo tumekusanyika hapa kwa ajili ya suala la afya ambapo tumelenga kuwasaidia Watanzania wenzetu wanaokumbwa na tatizo la afya ya akili, Takwimu zinaonyesha tatizo la afya ya akili limekuwa mtambuka na hatari zaidi ni kuwa kundi lililoathirika zaidi ni la watu wenye umri wa kati ya miaka 15 na 39 ambao ndio nguvu kazi ya taifa,”amesema Matundu.
Akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassimu Majaliwa, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete ameipongeza benki ya Exim kwa jitihada zake katika kuboresha huduma za afya nchini.
“Ninatoa wito kwa makampuni na taasisi nyingine kuiga mfano wa Benki ya Exim, Suala la Afya ya akili lazima lipewe kipaumbele na kila mtu, sio jambo la Serikali au wizara ya afya tu, bali pia makampuni, mashirika, wadau wa maendeleo, na jamii kwa ujumla kwa pamoja, tunaweza kuunda mfumo bora wa afya unaojumuisha kila mtu na kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma,” amesema Ridhiwani.
Amesema kuwa Katika jumla ya mikoa 28 nchini, mikoa mitano tu ndiyo ina vituo vinavyotoa huduma za afya ya akili zinazokidhi viwango, Ukubwa na hatari ya tatizo hili ni takwimu kuonesha kuwa kundi lililoathirika zaidi ni la wenye umri wa kati ya miaka 15 na 39 ambao ndio nguvu kazi ya Taifa na hivyo kuhitajika juhudi za ziada kuokoa kizazi hiki kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Tanzania.
“Jitihada hizi za Exim Bank zinaendana na malengo makubwa ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anafikia na kupata huduma bora za afya wakiwemo wagonjwa wa afya ya akili kwa kuboresha huduma za afya ya akili, benki inalenga kuchangia katika ujenzi wa mtandao wa jamii ambayo inaweza kufikia huduma kwa haraka, gharama nafuu, wakati wowote na mahali popote Tanzania.”amesema.
Hata hiyo Benki hiyo imetoa wito kwa mdau yeyote au taasisi ambao wanaguswa na changamoto hiyo na wangependa kuchangia kufanya hivyo kupitia akaunti maalumu yenye Jina: Exim Cares na Akaunti Na: 0010060253.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam