Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BENKI ya Exim Tanzania, moja ya taasisi kinara za kifedha nchini, leo imeadhimisha kumbukizi ya miaka 28 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa na kaulimbiu ya mwaka huu “Miaka 28 ya Kusonga Mbele Pamoja na Wewe.”
Sherehe hizo, zilizofanyika katika makao makuu ya benki hiyo, Exim Tower jijini Dar es Salaam zimewakutanisha menejimenti na wafanyakazi kwa ajili ya kutafakari safari ya benki hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 1997. Safari hii imejengwa juu ya ukuaji endelevu, ubunifu, na dhamira ya dhati ya kumuweka mteja mbele katika kila hatua.
Kutoka kuanza na tawi moja pekee katika Mtaa wa Samora, Benki ya Exim leo imepanuka na kuwa taasisi ya kimataifa yenye matawi nchini Comoro, Djibouti na Uganda. Hatua hii ya ukuaji inaonyesha uimara wa benki na kujitolea kwake katika kutimiza mahitaji ya wateja, huku falsafa yake ikijikita katika misingi ya Uwezo wa Kubadilika, Uhakika, Uadilifu, Utaalamu na Ari ya Kuhudumia Wateja kwa viwango vya juu.

Akizungumza na wafanyakazi wakati wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim Tanzania, Jaffari Matundu, alieleza maana ya kaulimbiu ya mwaka huu kwa kusema:
“‘Wewe’ katika kaulimbiu yetu ni heshima kwa wafanyakazi wetu hodari, ambao ndio moyo na roho ya benki, na pia kwa wateja wetu wanaotuamini kwa ndoto zao, fedha zao na maisha yao ya baadaye. Tunapoadhimisha miaka 28, hatuangalii tu tulichokijenga nyuma yetu, bali tunaelekeza macho mbele kwa yale makubwa zaidi ambayo bado tunaweza kufanikisha pamoja.”
Katika miaka ya karibuni, Benki ya Exim imefanya mageuzi makubwa ya kiteknolojia, yakiwemo maboresho ya mfumo wa msingi wa kibenki (Core Banking System) yaliyowezesha huduma bunifu zaidi na kuimarisha upatikanaji wa huduma kote nchini.
Huduma mpya zilizozinduliwa zimeendelea kuthibitisha msimamo wa benki kama taasisi bunifu inayoendana na mahitaji ya wateja. Baadhi ya huduma hizo ni Lipa Chapchap kwa wafanyabiashara na Elite Banking kwa wateja wa kifahari. Hivi karibuni pia benki imezindua huduma ya kipekee ya “Kopa KiBoss na Wafanyakazi Loan”, inayowawezesha watumishi wa umma kukopa hadi shilingi milioni 200, na marejesho ya hadi miaka 11, ikiwa ya kwanza katika sekta ya fedha nchini.



Akisisitiza nafasi ya ubunifu katika sekta ya kifedha inayobadilika kwa kasi, Bw. Matundu aliongeza:
“Kwa mifumo na ubunifu tulioanzisha, matarajio ya wateja wetu yameongezeka zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Ni jukumu letu kutambua mahitaji yao mapema, kuendelea kujifunza, kukua na kuboresha huduma zetu ili kwa pamoja tuijenge benki na mustakabali wa kifedha ambao kila mmoja wetu anaweza kujivunia.”
Kadri Benki ya Exim inavyoendelea na safari yake, malengo yake yako wazi: kuimarisha ukuaji, kupanua huduma zake, kuongeza ubunifu na kuimarisha huduma kwa wateja, sambamba na kuchangia maendeleo ya sekta ya fedha na taifa kwa ujumla.
Maadhimisho haya ya miaka 28 ni ushahidi wa safari yenye mafanikio na uthibitisho wa dhamira ya Benki ya Exim katika kujenga mustakabali bora wa kifedha kwa Watanzania na ukanda mzima.


More Stories
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao