January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Dunia yajitosa kusaidia ujenzi wa Reli ya kisasa na kukarabati Reli ya kati

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Benki ya Dunia imeahidi kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi unaoendelea wa  Reli ya Kisasa-SGR  na ukarabati wa Reli ya Kati-MGR, kutokana na umuhimu wa miradi hiyo katika maendeleo na uchumi wa nchi.

Ahadi hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, aliyeongoza ujumbe wa Benki hiyo, walipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa.

Bw. Belete alisema kuwa Benki ya Dunia ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Tanzania na kwamba imeamua kushiriki katika ujenzi wa miradi hiyo miwili ya reli pamoja na kwamba kipaumbele kikubwa cha nchi kwa sasa ni ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR.

Alibainisha kuwa timu ya wataalam kutoka Benki ya Dunia na Tanzania wakutane haraka kuchakata mahitaji ya miradi hiyo ili Benki itoe fedha za kuiwezesha nchi kutimiza malengo yake ya kukamilisha miundombinu ya reli hizo muhimu ambazo kukamilika na kuboreshwa kwake, kutasisimua uchumi, kuimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo, ndani na nje ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mawaziri wa Ujenzi na Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliishukuru Benki ya Dunia kwa utayari wao wa kusaidia ujenzi wa SGR na Reli ya Kati kutokana na umuhimu wake kwa Taifa kiuchumi na kijamii.

Pamoja na kujadili kwa kina kuhusu mradi wa Reli ya Kisasa SGR, kikao hicho, kilijadili pia masuala ya upatikanaji wa fedha za dharura kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua, na Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam-DART.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maanry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, anayesimamia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila, Viongozi wa Juu wa TRC, TANROADS, TARURA na DART.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kushoto), 
akifurahia jambo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete  wakati wa Kikao cha majadiliano kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kuhusu masuala kadhaa ikiwemo maombi ya Tanzania kwa benki hiyo, kufadhili Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na ukarabati wa Reli ya Kati (MGR), ambapo Benki hiyo imekubali kutoa fedha baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani za pande hizo mbili. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb)(katikati), akiongoza Kikao cha majadiliano kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kuhusu masuala kadhaa ikiwemo maombi ya Tanzania kwa benki hiyo, kufadhili Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na ukarabati wa Reli ya Kati (MGR), ambapo Benki hiyo imekubali kutoa fedha baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani za pande hizo mbili. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam, Kulia kwake ni Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohammed Mchengerwa, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayesimamia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila na kushoto kwake ni Mkurugenzi mkazi wa Benki hiyo, Bw. Nathan Belete na ujumbe kutoka Benki hiyo.Â