December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB yatoa mikopo ya kilimo ya tril. 1.26 mwaka 2023

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Mbeya

BENKI ya CRDB imeendelea kufungamana na wakulima nchini kwa kuendelea kutoa mikopo, ambapo hadi kufikia robo ya kwanza ya mwaka 2023 imetoa mikopo ya kilimo inayofikia trilioni 1.26 sawa na asilimia 43 ya mikopo yote ya kilimo inayotolewa na benki hapa nchini.

Kati ya mikopo hiyo bilioni 494 imeelekezwa kwenye mazao makuu ya kimkakati hivyo kusaidia zaidi ya vyama vya ushirika (AMCOS) vinavyofikia 472 kupata mikopo kwa ajili ya kuongeza tija kwenye uzalishaji wa kilimo ikiwa ni mikopo ya pembejeo, maghala, ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao, mikopo kwa ajili ya miradi ya ufugaji, uwekezaji kwenye misitu, uvuvi na biashara.

Wateja wa Benki ya CRDB wakipata maelezo kutoka kwa Meneja Mahusiano,Kilimo na Biashara Kanda ya Nyanda za Juu Gilbert Kyando (wa pili kulia)kwenye banda la CRDB lililopo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane katika Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Agosti 2, 2023 kwenye maonesho ya kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya, Meneja Mahusiano,Kilimo na Biashara Kanda ya Nyanda za Juu Gilbert Kyando amesema kwa kipindi cha miaka mitano ilyopita hadi kufikia mwezi Desemba 2022, Benki ya CRDB imetoa mikopo kwenye sekta ya kilimo inayofikia kiasi cha trilioni 3.6.

“Benki ya CRDB ndio benki pekee ya biashara iliyoanza kutoa mikopo nafuu zaidi kwenye sekta ya kilimo na kusaidia wakulima wadogo wadogo walioko kwenye vyama vya ushirika kupata uwezeshaji kwa riba ya asilimia tisa (9%) tu kwa mwaka,ambapo wakulima wadogo kupitia kwenye vyama vya ushirika wanaunganishwa na mfumo madhubuti wa kifedha kupitia mtandao imara wa CRDB,”amesema Kyando.

Pia amesema mkulima anaweza kupata huduma za kifedha kupitia CRDB Wakala na simu za mkononi hivyo, kujijengea tabia za kujiwekea akiba kupitia huduma rahisi zinazopatikana hadi vijijini.

Kyando amesema benki hiyo iko mstari wa mbele katika kufanikisha miradi mikubwa ya kimkakati,imeweza kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi ya umeme wa gesi – Kinyerezi (awamu ya I na ya II) – MW 150.

Pia usambazaji wa umeme vijijini kupitia REA,mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere Hydro – MW 2,115.

Upanuzi wa viwanja vya ndege,
ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) Dar-Morogoro-Dodoma-Tabora hadi Mwanza,
ujenzi wa barabara kuu zinazounganisha mikoa na wilaya zote za Bara na Visiwani kupitia wakandarasi mbalimbali wanaopewa kazi za ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.


Ujenzi wa miundombinu ya afya, elimu na usambazaji wa huduma muhimu ya maji mijini na vijijini kupitia mamlaka za maji.

Aidha amesema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kufufua ushirika kwa kutoa wataalam wanaosaidia kwenye shughuli za uendeshaji na kuongeza mitaji ili kuhuisha na kuujenga ushirika imara na imeweza kutoa mtaji wa bilioni 3.2 kwa TACOBA na bilioni. 7.0 kwa KCBL.

Hivyo kuwezesha benki hizo za ushirika kupata mtaji unaofikia kiasi cha bilioni 10.2 na kuweza kujiendesha kwa faida na tija zaidi.

“Tunatoa wito wa kuvikaribisha vyama vyote vya ushirika nchini kujiunga na benki hii ili viweze kujikwamua kiuchumi na kupata mazingira wezeshi kwenye sekta zote za kiuchumi,CRDB inautaratibu mzuri wa kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wa mazao yao (ndani na nje ya nchi),”.

Wateja wa Benki ya CRDB wakipata huduma ya Mobile Branch kwenye banda la CRDB lililopo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane kwenye Viwanja vya Mwakangale jijini Mbeya.

Sanjari na hayo amesema wakulima wengi wamekuwa hawatumii pembejeo sahihi katika uzalishaji wa mazao ya kilimo hivyo kupata mavuno hafifu na gharama kubwa za uzalishaji na kupata faida kidogo.

“Hali hii hupunguza kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo na uchumi wa nchi kwa ujumla,benki inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo kwa jumla (bulk procurement) ambapo utaratibu huu umesaidia kupunguza gharama za upataikanaji wa pembejeo kwa wakulima,”amesema Kyando.

Kyando amesema benki hiyo ikishirikiana na Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), imefanikiwa kubuni mfumo madhubuti wa kidigitali ili kurahisisha usambazaji wa mbolea za ruzuku.

“Wadau wote wanasajiliwa kupitia mfumo wa kidijitali (wanunuzi wakubwa, wasambazi na wakulima ambao ndio wanufaika wa mwisho wa mbolea za ruzuku) na taarifa zao zitahifadhiwa kwenye mfumo kulingana na maeneo wanapotoka, ukubwa wa mashamba yao, aina ya mazao na vyama au vikundi ambavyo wakulima wamejisajiliwa na unarahisisha upatikanaji wa mbolea zenye ubora kwa wakati na umepunguza na kuondoa tatizo la uingizaji wa mbolea zisizo na ubora,”.

Vilevile amesema benki hiyo ikishirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inaendelea kuwawezesha wajasiriamali wa awali, wa kati na wakubwa walioko Unguja na Pemba kupitia mpango maalum wa Inuka na Uchumi wa Buluu kwa kutoa mikopo ili waweze kuongeza mitaji yao kwenye shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda na biashara.

Katika mpango huo, zaidi ya bilioni 60 zinaendelea kutolewa kwa wanufaika wasiopungua 50,000 walioko Zanzibar ili waweze kuongeza mitaji kwenye miradi yao na kuongeza tija kwenye uchumi wa nchi.

“Benki ya CRDB pia inao mpango madhubuti wa utoaji mikopo maalumu ya zana bora za kilimo kwa kushirikiana na wadau wa usambazaji ikiwa ni pamoja na Hughes (New Holland), Reliance Group Ltd (Sonalika), ETC Agro (Mahindra), LonAgro (John Deere), Agricom (Kubota & Swaraj) na ZANA BORA Ltd,”.

Kadhalika amesema mikopo hiyo ni maalumu inalenga kuwainua wakulima na kufungua fursa kwa kuwawezesha na kuondoa masharti ya dhamana ambapo zana za kilimo zitakazonunuliwa kupitia utaratibu huu, ndio zitakuwa dhamana kuu ya mkopo kwa kuchangia kidogo kwa kutoa asilimia 25 ya thamani ya mashine itakayo nunuliwa na benki itaweza kutoa mkopo wa asilimia 75 inayobakia.