November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB kinara utoaji huduma za bima

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha

KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware amesema Benki ya CRDB imeonesha njia kwa kuwa benki ya kwanza nchini kujishughulisha na utoaji huduma za bima nchini, hivyo ana matumaini watafanya vizuri na kuwafungulia milango wengine.

Aliyasema hayo Mei 17, 2023 kwenye hafla ya kukabidhiwa Leseni ya Biashara Kampuni Tanzu ya CRDB Insurance na TIRA iliyofanyika jijini Arusha.

“Benki ya CRDB ndiyo mtoto wa kwanza kutoa huduma za bima nchini. Niseme ni mdau wa kwanza kufungua Kampuni Tanzu ya Bima. Sina mashaka na Benki ya CRDB kwenye hili, kwani imekuwa ikifanya mengi bila matatizo, hivyo naamini hata hili watafanya vizuri, na watakuwa ni mfano kwa wengine kutoa huduma hiyo” alisema Dkt. Saqware.

Dkt. Saqware alisema TIRA inafanya huduma ya bima kwa wananchi, hivyo kwa kuwapata Benki ya CRDB, watakuwa wamepata msaidizi mkubwa wa kutoa huduma hiyo, hivyo kuweza kushirikiana kwa pamoja kuwahudumia wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela alisema wamejipanga kutoa huduma bora za bima, kwani wana uzoefu wa miaka 15 kwenye shughuli za bima, na wana uwezo wa kuisadia Serikali kuongeza Pato la Taifa (BDP) kupitia huduma za bima kutoka asilimia 1.68 hadi asilimia tatu ama zaidi ya hapo.

“Mpaka tunapata leseni hii leo, Benki ya CRDB inayo historia kubwa ya kufanya biashara ya bima, kwani takriban miaka 15 iliyopita imekuwa ikiifanya kwanza kwa kupitia kwa iliyokua kampuni tanzu ya CRDB Micfrofinance na baadae tulitoa huduma hizi kama wakala wa bima tukiitwa CRDB Insurance Broker.

“Katika lugha rahisi kinachofanyika leo ni kuwa tumeweza kuongeza uwezo wetu wa kutoa kuduma hizi ambapo kwa sasa hatutokua mawakala tena bali tutakua ni kampuni ambayo inakwenda kutoa huduma za bima yenyewe kama ambavyo yanafanya makampuni mengine. Ingekua ni mtaani kule, basi badala ya kuwa dalali wa kuuza nyumba za watu wengine sasa dalali yule anajenga nyumba zake na kuuza mwenyewe” alisema Dkt. Saqware.

Kwa leseni hiyo, kampuni ya CRDB Insurance itajikita kutoa bima za
vyombo vya moto (kubwa na ndogo),
bima za majengo (property insurance), bima za wakandarasi, bima za mazao ya kilimo haswa pale inapotokea mabadiliko ya hali ya hewa, bima za kusafirisha fedha, bima za kukinga biashara dhidi ya hasara, bima za safari, bima za kukinga mabenki na bima za usafiri wa majini.

“Kampuni tanzu ya CRDB Insurance imekuja wakati muafaka kwani itakwenda kuongeza nguvu katika kufanikisha utekelezaji wa mkakati wa Serikali katika huduma za fedha yaani Financial Sector Master Plan 2030, ambapo Serikali imeweka malengo kuwa ifikapo mwaka 2030 basi, walau nusu ya Watanzania wawe wanapata na kutumia huduma za bima.

“Tutahakikisha tunafanikisha hili kwa kutoa elimu kwa wananchi kupitia programu mbalimbali ili kuhakikisha kuwa huduma hizi za bima zinawafikia na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi kwani wapo wengi ambao wamepoteza mali zao walizochuma kwa jasho kwa kukosa tu elimu ya bima” alisema Nsekela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Wilson Mnzava ameahidi kutoa huduma bora ya bima ikiwemo zile za lazima, na zile za kilimo na biashara. Hivyo wakulima, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali na makundi mengine, wajipange kupata huduma bora kutoka CRDB Insurance.

Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware (wa pili kulia) akikabidhi Leseni ya utoaji Huduma za Bima kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto) kwenye hafla ya makabidhiano ya leseni hiyo yaliyofanyika jijini Arusha Mei 17, 2023. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya CRDB Insurance Wilson Mnzava (kushoto), na
Mjumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB, na CRDB Insurance Company Limited, Gerald Kasato (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware (katikati) akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya Leseni ya utoaji Huduma za Bima kwa Kampuni Tanzu ya CRDB yaliyofanyika jijini Arusha Mei 17, 2023. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya CRDB Insurance Wilson Mnzava (kushoto),
Mjumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB, na CRDB Insurance Company Limited, Gerald Kasato (wa pili kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation Tully Mwambapa. (Picha na Yusuph Mussa).
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela (katikati), akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya leseni ya utoaji huduma za bima kwa benki hiyo yaliyofanyika jijini Arusha Mei 17, 2023. Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya CRDB Insurance Wilson Mnzava (kushoto), na Kamishna wa TIRA Dkt. Baghayo Saqware (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Tanzu ya CRDB Insurance Wilson Mnzava (kushoto),
akizungumza
kwenye hafla ya makabidhiano ya leseni kwa benki hiyo kutoka TIRA yaliyofanyika jijini Arusha Mei 17, 2023. Wengine ni Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware (kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Group Abdulmajid Nsekela (katikati). (Picha na Yusuph Mussa).
Maofisa wa Benki ya CRDB, wakishuhudia makabidhiano ya Leseni ya utoaji Huduma za Bima kutoka TIRA kwenda kwa Kampuni Tanzu ya CRDB Insurance. Hafla hiyo imefanyika Mei 17, 2023 jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa).
Maofisa wa Benki ya CRDB, wakishuhudia makabidhiano ya Leseni ya utoaji Huduma za Bima kutoka TIRA kwenda kwa Kampuni Tanzu ya CRDB Insurance. Hafla hiyo imefanyika Mei 17, 2023 jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa).