Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Exhahudi Kigahe amesema bei za vyakula kwa mwezi Disemba zimeendelea kupanda kutokana na vita inayoendelea baina ya Nchi ya Urusi na Ukrain huku akibainisha kuwa sio tu Tanzania bali na mataifa mengine huku majanga mengine ikiwa ni Ukame ulioathiri mazao ya chakula
Kihage ameyasema hayo jana Jijini Dar es salaam wakati akieleza mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi Disemba 2022 na kusema kuwa mfumuko wa bei nchini Tanzania ni wa kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na nchi jirani ambapo Tanzania mfumuko wa bei kwa mwezi Novemba ni asilimia 4.9, Kenya asilimia 7.38, Uganda asilimia 10.6 na Rwanda asilimia 21.7.
“Mwenendo wa bei za bidhaa umeendelea kuonesha tofauti za viwango vya bei za jumla na rejareja ambapo bei za baadhi ya bidhaa hasa za vyakula zimeongezeka kutokana na kupungua kwa uzalishaji kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022.”
Aidha Kigahe amesema pamoja na upungufu katika uzalishaji kutokana na hali ya hewa isiyoridhisha kwenye maeneo mengi nchini na nchi jirani,mahitaji ya bidhaa za vyakula kwenye nchi jirani yameongezeka na hivyo kuongeza bei.
“Kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na athari zake kwenye kiasi cha mavuno muhimu ya chakula kama mchele, mahindi, maharage na viazi mviringo; mahitaji ya bidhaa hizo kwenye nchi jirani yamekuwa makubwa kuliko uzalishaji, hivyo kuchangia kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula nchini na nchi jirani.”
Kigahe amesema bidhaa za vyakula zilizoathirika zaidi na upungufu wa mvua na hivyo bei zake kupanda ni pamoja na maharage na viazi mviringo.
“Bei ya maharage kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 2,200 hadi 3,650 kwa kilo. Bei ya chini imepungua kwa Shilingi 260 kwa kilo ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei ya juu imepanda hadi Shilingi 3,650 kutoka Shilingi 3,250 mwezi Novemba. Bei ya chini inapatikana katika Mkoa wa Katavi na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Manyara na Tabora. ”
“Bei ya Viazi Mviringo kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 688 na 1,875 kwa kilo. Bei ya juu ya Viazi Mviringo imepanda kwa Shilingi 375 ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei ya chini ipo katika Mikoa ya Njombe, Songwe na Mbeya na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Mara na Dar es Salaam. ” Alisema Kigahe.
Kigahe amesema Bei ya mafuta ya kupikia ya Alizeti kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 4500 na 7,750 kwa lita. Vile vile, bei ya mafuta ya kupikia ya Mawese (Korie na Safi) kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 5,000 na 7,600 kwa lita.
“Bei ya chini ya mafuta ya kupikia ya Alizeti ipo katika Mikoa ya Manyara, Iringa, Tabora na Dodoma na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Mtwara, Mara, Kigoma, na Ruvuma.”
Kuhusu Mchele, Kigahe amesema bei ya mchele kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 2,200 na 3,500 kwa kilo. Bei ya chini na ya juu imepanda kutoka 2,000 na 3,200 kwa kulinganisha na mwezi Novemba.
Mikoa yenye bei ya chini ni Katavi na Ruvuma na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Kagera, Manyara na Arusha. Kigahe amesema Bei ya nondo mm 12 kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 22,650 na 28,000 ambapo bei ya nondo mm 12 imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei za chini zipo katika Mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Katavi, Kagera, Iringa na Njombe.
“Bei ya nondo mm 10 kwa mwezi Desemba ni kati ya Shilingi 18,000 na 22,500. Bei ya nondo mm 10 imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba. Bei za chini zipo katika Mikoa ya Iringa, Kilimanjaro na Mara na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Tabora, Kagera, na Songwe.”
Kwa upande wa Saruji, Kigahe amesema Bei ya saruji kwa mwezi Disemba ni kati ya Shilingi 15,000 na 24,000 kwa mfuko wa kilo 50. Bei hiyo imeonesha uhimilivu ikilinganishwa na mwezi Novemba ambapo Mikoa yenye bei ya chini ni Tanga, Dar es Salaam, Mtwara, na Pwani na bei ya juu ipo katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Katavi.
Kigahe amesema Serikali kupitia Sera ya Maendeleo ya Viwanda inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Viwanda vinavyozalisha bidhaa za sabuni hususan sabuni za maji na sabuni za unga ikiwa ni pamoja na kurahisisha taratibu za uingizaji wa malighafi muhimu zinazotumika katika uzalishaji wa sabuni kutoka nje ya nchi.
Kigahe amesema Wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji wa taarifa za uhakika za bei za bidhaa na masoko, kufanya uchambuzi na kusambaza kwa wadau.
“Tutaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kupitia Idara mpya ya Uwekezaji Viwanda na Biashara iliyoanzishwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini tupate taarifa za kuaminika kwa wakati kutoka maeneo yote nchini.”
Aidha, Kigahe amewahimiza Wafanyabiashara kote nchini kuendelea kuzingatia misingi ya ushindani wa haki katika kufanya biashara ili kuunga mkono jitihada za Serikali za kukuza uchumi kwa manufaa ya Wananchi wote ambapo Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha uzalishaji wa mazao ya chakula ili kudhibiti mfumuko wa bei nchini.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua