July 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bei ya mafuta yazidi kushuka

Na Mwandishi Wetu

BEI za jumla na rejareja za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta yaliyopokelewa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la Aprili 1, mwaka huu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dar es Salaam jana na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje, ilieleza kwamba bei hizo zitaanza kutumika kuanzia leo.

Kwa mujibu wa EWURA mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani yanatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji (BPS Premium)

Taarifa hiyo ilieleza kwamba Mei, 2020 bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa sh. 219/lita (sawa na asilimia 10.50), sh. 143/lita (sawa na asilimia 7.17) na sh. 355/lita (sawa na asilimia 18.47), mtawalia.

Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua kwa sh.  218.59/lita (sawa na asilimia 11.14), sh. 142.25/lita (sawa na asilimia 7.63) na sh.354.09/lita (sawa na asilimia 19.69), mtawalia.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli katika mkoa wa Tanga zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la Aprili 1, 2020.

Kwa mwezi Mei 2020, bei za rejareja za Petroli na Dizeli kwa Mikoa ya Kaskazini (yaani Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara) zimepungua kwa sh. 463/lita (sawa na asilimia 21.88) na sh. 377/lita (sawa na asilimia 18.21), mtawalia.

Aidha, kwa kulinganisha na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli na dizeli zimepungua kwa sh. 461.82/lita (sawa na asilimia 23.19) na Shilingi 375.82/lita (sawa na asilimia 19.33), mtawalia.

“Bei za mafuta ya taa kwa Mikoa ya Kaskazini zitaendelea kuwa zile zilizochapishwa katika toleo la Aprili 1, 2020 kwa sababu hakuna shehena ya bidhaa hiyo iliyopokelewa nchini kupitia bandari ya Tanga kwa mwezi Aprili 2020,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba kwa mwezi Mei 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya dizeli katika mikoa ya kusini (yaani Mtwara, Lindi na Ruvuma) hazitabadilika ikilinganishwa na toleo lililopita Aprili 1, 2020 kutokana na kuwa hakuna shehena ya Dizeli iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara.

“Hata hivyo, bei za mafuta ya petroli zimepungua ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita. Kwa mwezi Mei 2020, bei za jumla  na rejareja za petroli zimepungua kwa sh. 129/lita (sawa na asilimia 5.67) na sh. 128.14/lita (sawa na asilimia 5.99), mtawalia.

Kwa kuwa hakuna mafuta ya taa katika bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za mafuta ya taa kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutokea Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika,” ilieleza taarifa hiyo.

EWURA  imesisitiza kwamba bei kikomo za mafuta kwa eneo husika, zinapatikana pia kupitia simu za mkononi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.