November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Batuli: Wasanii tuwaondoe watoto mitandaoni

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MSANII wa filamu hapa nchini, Yobnesh Yusuf maarufu kama ‘Batuli’, amewataka Wasanii kuacha tabia ya kuwapost watoto zao kwenye mitandao ya kijamii kwani hawawezi kuhimili mambo ambayo wazazi wao wanakumbana nayo katika mitandao hiyo.

Akitoa ujumbe huo kupitia kwenye Ukurasa wake wa Instagram Batuli amesema, mitandao ya kijamii ina vurugu sana ikiwemo matusi, kashfa hivyo itawaaribu tabia na kuwajengea tabia zisizofaa kwenye jamii ya Kitanzania.

“Tujifunze kupitia jana yetu, leo yetu haina uhakika na kesho yetu ni majaaliwa. Nadhani kuna haja ya kuwaondoa watoto wetu kwenye Mitandaoni ya Kijamii. Ni wadogo sana kuhimili tunayohimili sisi wazazi wao kwenye Mitandao yetu ya Kijamii, Mikiki Mikiki, Vurugu na Kashfa za Mitandao yetu sisi wenyewe na utu uzima wetu. Kuna wakati inatupotezea uelekeo, kuhimili haya yanahitaji moyo wa Ujasiri na nguvu kutoka kwa Mungu.

“Wakati wao utafika watatumia kila kitu watakacho, ila kwa umri huu ambao wanajenga kesho yao nadhani tuwaepushe na hizi hasada za Dunia, Safari ya Watoto wetu bado ni ndefu Sana, Wanahitaji utulivu wa akili na mwongozo mwema kutoka kwetu sisi wazazi wao, Kama mzazi naumia sana mtoto wa mwenzangu akipitia ambayo hapaswi kuyapitia kwa umri wake na uwezo wa kumuepusha nayo upo.

“Baadhi yetu tumejilea kupitia Sanaa, Tumepitia mengi hadi kufikia hapa tulipo na mifano hai kupitia sisi ipo na jamii imeona. Tusikubali watoto wetu wapitie njia zetu mbovu, njia zenye misukosuko mingi Sana, ni wazi kila mtu ana maamuzi yake ya kuishi ila Watoto wetu ndio tegemeleo letu la kesho, Dunia iliyotulea sisi sio hii inayowalea Watoto wetu bila elimu iliyonyooka na historia safi huko waendako ni pagumu Sana. Tuwawekee ulinzi wa kutosha ila Mitandao ya Kijamii ni sawa na jahanam kwa watoto wetu, mnisamehe kwa nitakao wakwaza,” ameandika Batuli.