November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bashungwa, Ulega kuunganisha COSOTA, BASATA

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa pamoja na Naibu wake Abdalah Ulega wameweka wazi mikakati mikuu wanayoanza nayo katika kusimamia Wizara hiyo ikiwemo kuunganisha Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Viongozi hao wametoa kauli hiyo jana walipotembelea Bodi ya Filamu Tanzania katika mwendelezo wa ziara yao ndani ya Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Habari, wakiwa wameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas.

Akizungumza baada ya kukao hicho, Waziri Bashungwa amesema, licha ya kuunganisha COSOTA na BASATA lakini pia watahakikisha wasanii wanapata maslahi yao wakiwa hai na kuwafikia hata wale walio Mikoani, kurejesha Tuzo za Muziki na Filamu pamoja na kukuza ajira katika sanaa.

Bodi hiyo inatakiwa Kamati ya utetezi wa haki ya wasanii inafanya kazi kwa ufanisi na ubunifu kwani hadi sasa Wizara hiyo haijaridhishwa na utendaji wake kwani wanahitaji mabadiliko haraka sana.

“Tunataka kuwe na utetezi wahaki za wasii kuanzia wanapokuwa hai ili afaidi matunda ya kazi yake na si kusubiri hadi mtu afe, ninachotaka kuona ni Kamati hii inafanya kazi kwani Serikali inakusudia kuziweka sehemu moja taasisi za Cosota na Basata ili kuondoa usumbufu kwa wasanii na tayari jengo linatafutwa ili kufikia malengo ya kuwapata wasanii wote mpaka ngazi za chini kupitia maafisa utamaduni Mikoa na Wilaya ,” amesema Bashungwa.

Lakini pia amewaangiza kuacha kuwaachia wasanii kuhangaikia masoko bali washirikiane kwa pamoja ili kuhakikisha wanawatafutia masoko ya ndani na nje.

“Nimehangaika sana nilipokua Waziri wa viwanda kuhakikisha wasanii wanapata masoko na sasa tunakusudia tunalinda urithi wa kazi za wasanii na kazi za wasanii wetu ili kupata masoko na kuwaunganisha katika nyanja za Kitaifa na kimataifa,” amesema Bashungwa.

Pia Waziri huyo amesema sasa ni wakati wa kuzirudisha tuzo za filamu na muziki za kitaifa ili kurejesha ari ya wasanii katika kazi kwawkutambua mchango wao pamoja na kuanzishwa kwa tuzo za kimataifa ili kutangaza nchi na utalii wake.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Abdalah Ulega amesema, wanasuka mkakati maalum utakaohakikisha soka linapewa kipaumbele kwa kuweka muunganiko wa UMITASHUMTA, UMISETA kwa watoto ili kupika vipaji.

“Tunataka tuwe na vituo ‘academy’ za sanaa kuanzia chini ili kuibua na kuendeleza vipaji. Lakini pia ni lazima kuhakikisha vitengo vyote vya Taasisi ya bodi inasimama imara katika ufuatiliaji, udhibiti, kuhakikisha filamu zina ubora ili kuja na viwango vya kuziwezesha filamu ziwe za kimataifa,” amesema Ulega.

Pia ameahidi kutekeleza kikamilifu ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. john Magufuli ya kuzalisha ajira milioni 8 na ukiangalia Januari mpaka Desemba mwaka huu tayari kuna ajira 25,000 hivyo wanahitaji kutumia sekta hiyo kutoa ajira nyingi zaidi ili kufikia malengo.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amewaita wabunifu wote wa Mifumo ya kuuza Filamu, Muziki na wabunifu kwa njia za kidigitali katika kikao cha kuonesha mifumo hiyo inavyofanya kazi kwa lengo la kusaidia kupatikana kwa namna bora itakayosaidia kusambaza kazi za wabunifu nchini.

Kikao hicho kitafanyika kesho Desemba 17 ambapo kila mbunifu atapewa fursa ya peke yake kueleza namna mfumo wake unavyofanya kazi.