Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema serikali haitafumbia macho timu wala taasisi yoyote itakayobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwenye michezo ili kupata ushindi.
Bashungwa ametoa kauli hiyo Bungeni jana alipotoa jibu la nyongeza kufuatia majibu yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi kuhusiana na vitendo hivyo vya Rushwa.
Amesema, Wizara yake inapambana kwa nguvu zote na vitendo vya rushwa na wanashirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinavyohusika kupambana na rushwa huku wakiendelea kuweka mazingira ya michezo kukua bila kuwepo na rushwa.
Waziri huyo alisema kuwa, serikali yao haitafumbia macho taasisi, timu wala shirika lolote katika michezo ambalo litatumia rushwa kujipatia ushindi au manufaa yoyote.
“Serikali kupitia Wizara ya Michezo ninayoiongoza tunapambana na rushwa kwenye michezo kwa nguvu zote na tunashirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ya michezo nchini kukua bila kuwepo kwa mazingira ya rushwa, niwahakikishie Serikali haitofumbia macho timu inayotumia rushwa kujipatia ushindi” amesema waziri huyo.
Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi lililohoji ni kwa kiasi gani Serikali inakabiliana na kudhibiti vitendo vya rushwa vilivyoonekana kukithiri kwenye mchezo wa Ndejembi amesema, serikali inatambua kuwepo kwa vitendo vya rushwa hasa kwenye soka jambo linaloathiri maendeleo ya mchezo huo na kuikosesha serikali mapato.
Amesema, Serikali kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekuwa ikipambana na vitendo hivyo kwa kufanya uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya viingilio katika mechi mbalimbali na kubaini mianya ya rushwa.
Baada ya kubana mianya hiyo, mapato yaliongezeka hadi kufikia milioni 206 kwa watu 50235 kwa watu waliokata tiketi katika mchezo wa Machi 2019 ukilinganisha na mapato ya Sh 122 milioni kwa watu 47,499 waliokata tiketi kwa mechi iliyochezwa Januari 2019 kwenye uwanja huo.
“Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya michezo nchini, mwaka 2016 TAKUKURU iliunda timu maalum ya uchunguzi kufuatilia na kuchunguza vitendo vya rushwa katika michezo ambapo kesi tatu zimefunguliwa mahakamani na tuhuma saba zinaendelea kuchunguzwa, na semina imeendelea kutolewa kwa watendani mbalimbali ikiwemo waamuzi,” amesema Ndejembi.
Kufuatia jambo hilo, ameiagiza TFF, wasimamizi wa soka na viwanja vya michezo waruhusu na kushirikiana na TAKUKURU kuweka matangazo ya kukemea rushwa kwenye soka na michezo kwa ujumla.
Ngejebi amesema kuwa, hadi sasa serikali imeshachukua hatua kadhaa watuhumiwa waliobainika na kosa la rushwa na wataendelea kuwashughulikia na kwakua sasa nchi ipo kwenye maendeleo ya Teknolojia TFF wanatakiwa kutumia mifumo ya kisasa ya uuzaji wa tiketi
Akijibu swali la nyongeza na Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba kuhusiana na tuhuma za Nahodha wa timu ya Prisons, Benjamin Asukile ya kudai kutaka kupewa milioni 40 na Yanga katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho ambao Yanga ilipata ushindi wa goli 1-0 na kwenda robo fainali, Ngejebi amesema kuwa, ni lazima ifike hatu timu zikubali pale zinapopoteza mechi.
Amesema kuwa, kwa sasa imekuwa tabia na viongozi na wachezaji kuzihutumu timu zinazowafunga kwa halali hivyo ni lazima jambo hilo likomeshwe na kwa sasa tayari tuhuma hizo zimeshaanza kufanyiwa kazi ili kupata ukweli.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025