January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bashungwa ampongeza Mtaka, ataka Wakuu wa Mikoa kuiga ujenzi Soko la Machinga

Na Zena Mohamed, TimesMajira Online, Dodoma.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),Innocent Bashungwa amempongeza Mkuu wa Mkoa Dodoma Anthony  Mtaka kwa utaratibu mzuri aliotumia kuboresha zoezi la upangaji wa machinga kulingana na mazingira ya maeneo yao.

Huku akiwataka Wakuu wa Mikoa yenye Halmashauri zenye hadhi ya Majiji kutumia mbinu inayotumika katika ujenzi wa Soko la Wafanyabiashara wadogo (Machinga Complex) katika eneo la Bahi Road jijini Dodoma ili kuboresha zoezi la upangaji wa machinga kulingana na Mazingira ya maeneo yao.

Bashungwa ameyasema hayo jijini hapa leo  wakati wa ziara yake na wakuu wa mikoa, Makatibu Tawala, na Wakurugenzi wa mikoa yenye hadhi ya majiji kutembelea ujenzi wa eneo hilo ambapo amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametambua sekta ya machinga kuwa rasmi hivyo kwa sasa wanaenda na maono yake ya kuhakikisha wanajengewa mazingira rafiki kwa kazi zao.

“Napongeza ubunifu uliofanyika kwenye soko hili la machinga na namna jiji lilivyotafsiri maono ya Rais kwa kubuni masuala haya hii ni fursa kwa viongozi wengine wa mikoa yenye hadhi ya majiji kama Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya kujifunza kwa gharama ndogo hapa hapa nchini,

“Tungeweza kwenda nje ya nchi kubuni kitu ambacho tunaweza kujifunza sisi wenyewe hivyo tunajivunia suala hili na wakuu wa mikoa, makatibu Tawala na wakurugenzi nimewaomba mje hapa ili kutafsiri kwa vitendo kwenye ngazi za mikoa maana yapo mambo makubwa tunaweza kufanya, hivyo tumieni matamko ya viongozi na maono yao kufanya haya,”amesema.

Hata hivyo amewataka viongozi hao kupeleka elimu waliyojifunza kwenye soko hilo kwenye maeneo yao na kuhakikisha wanawashirikisha machinga kwenye ujenzi wa miradi hiyo ambayo itatekelezwa kwenye mikoa yenye hadhi ya majiji nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema wamejifunza kupitia mradi huo na kuahidi kuwa  watazingatia maelekezo waliyoyapata hapo na kwamba watatimizi dhamira ya Rais ya kuwawekea wamachinga katika mazingira rafiki na kuwafanya watambulike.

“Sasa  tukuombe kufanyia marekebisho bajeti zetu ili kuweka mpango huu hususani kwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2022/23 ili tuweze kulikamilisha suala hili kama ilivyokusudiwa,”amesema Homera.