Na Jackline Martin, TimesMajira Online
SERIKALI kupitia baraza la taifa la sanaa nchini (BASATA), limesema litaendelea kufanya kazi kwa kufuata muongozo wa uendeshaji kazi za sanaa.
Lengo la kufanya hivyo ni, kuzingatia maadili Ili Kupata taifa lenye Vijana wenye vipaji wanaoendana na kufuata maadili katika kazi za sanaa.
Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es salaam, na Afisa sanaa Mwandamizi kutoka BASATA, Agustino Makame
wakati wa kutangaza msimu wa 14 wa mashindano ya Bongo Star Search (BSS),ulioenda sambamba na kaulimbiu isemayo ‘Kipaju chako, Mtaji wako’.
Makame alisema moja ya jukumu la Basata ni kuhakikisha inashirikiana na wadau katika kufufua na kuendeleza vipaji vya watanzania hasa Vijana ikiwa ni pamoja na kusisitiza umuhimu wa uwekezaji katika sanaa.
“BASATA tumeshirikiana nao mwanzo hadi kufikia leo hii na kwa mwaka huu, wamekua na ubunifu mkubwa hasa kuongeza mkoa mmoja ili kuendelea kuibua vipaji vya wasanii nchini,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko kutoka star times ambao ni wadhamini wa BSS, David Malisa alieleza BSS imelenga kuibua vipaji vya Vijana ambavyo
huvitumia kujiingizia vipato binafsi na hivyo kushiriki kukuza uchumi wa nchi.
“Kila mwaka ambao tumekuwa tukishirikiana nao, BSS imekua ikikua Kila siku na imezidi kuwa kubwa hasa kiuwezo na utafutaji vipaji,” alisema Malisa.
Pia, alisema BSS msimu wa 14 ni kubwa sana kwani vipaji vimepikwa hivyo aliwapongeza kwa kuendelea kuibua vipaji, hivyo amewataka washirika wengine
kuweza kuunga mkono ndoto za waanzilishi wa BSS ya kuibua vipaji vya wasanii hao.
Naye Mratibu wa mashindano hayo, Rita Paulsen alibainisha kuwa katika fainali za Msimu huu wamefanikiwa kuongeza mkoa na kupata idadi kubwa ya washiriki wanawake.
“Kupitia usaili wa msimu huu, vijana zaidi ya 5,700 wamepita kwenye usaili wetu, tunaenda kufikia kwenye Top 6, na bado mchakato unaendelea.
“Mkoa tuliouongeza kwa mwaka huu ni Mkoa wa Kigoma, kwani mkoa huu tuliwahi kwenda mda mrefu na kufanikiwa kumpata msanii Msechu hivyo tumeona kuna haja ya kuongeza mkoa huu ili kuzidi kuibua vipaji vya wasanii wengine”
Katika mashindano hayo mshindi wa kwanza atapata shilingi Milioni 20 na Kiwanja Cha kujengea nyumba Cha square Mita 500, ambapo aliwasihi wadau wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi zawadi.
Hata hivyo alisema, fainali za BSS zinatarajiwa kufanyika Januri 27 mwaka huu, katika ukumbi wa Warehouse Masaki kuanzia saa 12 Jioni.
Alitaja Maduka yatakayouza tiketi ni startimes, Mlimani City, Mikocheni, Kitambaa Cheupe, Palm Village,
Warehouse Masaki, Shishi Food, na kupitia Nilipe APP.
More Stories
Startimes yazindua makala ya China, Africa
Mwanasheria wa Katavi aliyetimkia kwenye muziki achaguliwa tuzo za MIEMMA
Coca-cola ‘Kitaa Food Fest’ yahitimishwa kwa mafanikio