March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barua ya Mwanafunzi,Prof.Mbarawa atoa maagizo LATRA

Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameiagiza  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuhakikisha zoezi la kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu (makondakta) kwenye mabasi linafanywa kwa kasi katika miji yote Nchini, na kutoa adhabu kali kwa mujibu wa Sheria kwa madereva na makondakta watakaobainika kuwanyanyasa wanafunzi.

Prof.Mbarawa ametoa maagizo hayo jijini hapa leo Februari 4,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua za serikali kuboresha usafiri wa wanafunzi katika maeneo ya mijini.

Hatua hiyo imekuja kutokana na Barua ya Mwanafunzi  Mariana Mirindima kwa Serikali ambapo ameeleza kwamba makondakta wamekuwa wakigoma kuwabeba wanafunzi kwa kisingizio cha kibiashara wakidai kuwa wanafunzi hawalipi nauli kamili. 

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wanalazimika kusimama barabarani kwa muda mrefu wakisubiri usafiri, wanachelewa kufika shuleni, na wakati mwingine wanashindwa kabisa kufika shuleni. Hali hii inawatia hofu wanafunzi, inawachosha, na inaathiri masomo yao, pamoja na usalama wao kama watoto. 

Alieleza pia kuwa wanafunzi wanategemea sana daladala kama njia yao kuu ya usafiri, hivyo wanapoachwa njiani au kunyimwa huduma wanakuwa kwenye mazingira hatarishi, na kunyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu kwa usalama. 

Hivyo, mwanafunzi Mariana akaomba, kwa niaba ya wanafunzi wengine, Wizara yangu ichukue hatua stahiki dhidi ya vitendo wanavyofanyiwa wanafunzi na watoa hudumaza daladala (Wamiliki, Madereva na Makondakta). Kisha akamalizia kwa kusema anawasilisha barua hiyo akiwa na matumaini makubwa kwamba sauti ya wanafunzi itasikilizwa na itafanyiwa kazi.

“Nimeona video clip kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ambapo binti aliyejitambulisha kwa jina la Mariana Eric Mirindima ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Shule ya Sekondari Jangwani akiwasilisha barua yake iliyoeleza changamoto wanazokutana nazo wanafunzi wanaotumia usafiri wa mabasi ya mijini, maarufu kama daladala. 

“Kwanza, ninamshukuru mwanafunzi huyo namzazi wake aliyesimamia kwa ujasiri uamuzi huu wa kupaza sauti na kutoa mrejesho kuhusu changamoto hii kupitia mitandao ya kijamii. Kwakufanya hivyo, kijana huyu na mzazi wake wametimiza wajibu wao wa msingi wa kuipa Serikali na Mamlaka zote husika mrejesho unaopaswa kufanyiwa kazi. Na kwa hakika sauti ya wanafunzi imesikilizwa na itafanyiwa kazi,”amesema.

Kutokana hayo Waziri huyo pia ameiagiza LATRA  kiumarisha udhibiti wa nauli maalumu za wanafunzi, staha ya huduma na usalama wao kwa wakati wote,

 Kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma, na watumia huduma wajue haki na wajibu wa kila mmoja,kuhakikisha  Treni za Abiria, Daladala zote Nchini pamoja na Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi jirani zimeandikwa namba za bure ili abiria waweze kupiga LATRA 0800 11 00 19 na 0800 11 00 20 na
Kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushtukiza kwenye vituo vya daladala hasa nyakati za asubuhi na jioni kuhakikisha wanafunzi wanapata usafiri.

Pamoja na hayo Prof.Mbarawa aliwaomba Watanzania, na abiria kwa ujumla kushirikiana kuwatetea wanafunzi wanaponyanyaswa na mtu yeyote. Mnaweza kutuma ushahidi wa picha au sauti kwa namba ya LATRA WhatsApp 0681 300 800.