January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barcelona yaachana na Messi

BARCELONA, Uhispania

KLABU ya Barcelona imesema mshambuliaji wake nyota, Lionel Messi hatakuwepo klabuni hapo “kwa sababu ya vizuizi vya kifedha na utawala”.

Messi, mwenye umri wa miaka 34 raia wa Argentna, amekuwa mchezaji huru tangu Julai mosi mwaka huu, wakati mkataba wake ulipomalizika. Amedumu katika klabu hiyo takribani miaka 21 akiwa na magoli 672.

Hata hivyo, alikubali kusaini mkataba mpya uliokuwa na kipengele cha kupunguza mshahara, wiki mbili baada ya mkataba wa awali kumalizika. Lakini hali hiyo ilitegemea zaidi klabu hiyo kuuza wachezaji ili kumudu mshahara wake.

“Pande zote mbili zimeelezea kusikitika kutokana na matakwa ya mchezaji na klabu kutotimizwa,” imesema taarifa ya klabu hiyo.

Barcelona imesema Messi alikuwa tayari kuongeza muda kusalia klabuni hapo alipodumu kwa miaka 21 kwa kusaini mkataba mpya siku ya Alhamisi, na kulaumu La Liga kwa kutofanya hivyo.

Tayari alifikia makubaliano ya kukaa na timu hiyo hadi 2026 – lakini La Liga inasema klabu lazima ipunguze mshahara kabla ya yeye na mchezaji yeyote yule mpya kusajiliwa.

“Licha ya Barcelona na Lionel Messi kufikia makubaliano na nia ya wazi ya pande zote mbili kutia saini mkataba mpya leo, hii haiwezi kutokea kwa sababu ya vizuizi vya kifedha na kiutawala (kanuni za Ligi Kuu ya Hispania, La Liga),” klabu imesema.

“FC Barcelona inatoa shukrani za kipekee kwa mchezaji huyo kwa mchango wake katika kukuza klabu na inamtakia kila la kheri katika siku zijazo kwenye maisha yake ya binafsi ya soka.” Imeongezeka taarifa ya Barcelona.

Lionel Messi alianza kuichezea klabu ya Barcelona mwaka 2000, amefunga magoli 672 na kushikilia rekodi ya mfungaji wa muda wote wa klabu hiyo.