Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online
MKOA wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa yenye mitandao mirefu ya barabara katika maeneo ya mijini na vijijini ukiwa na mtandao wa kilometa 5,220.02 zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Katika kilometa hizo barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami ni kilometa 38.132, changarawe kilometa 1,406.38 huku udongo kilometa 3,775.51.
Ujenzi wa barabara hizo zinazosimamiwa na TARURA zinatekelezwa kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 lengo kuu ikiwa ni kuwaondolea wananchi changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo yao.
Miongoni mwa ahadi ya CCM kwa watanzania kipindi cha kampeni wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kiliahidi iwapo kitapewa ridhaa ya kuunda Serikali moja ya mambo itakayowapa kipaumbele ni uimarishaji wa miundombinu ya barabara.
Katika Ilani hiyo ibara ya 57 inaeleza kuwa nanukuu; “Kwa kutambua umuhimu wa kuendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi katika kuwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii mijini na vijijini,”.
“Chama Cha Mapinduzi katika kipindi cha miaka mitano ijayo kitahakikisha miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi inaboreshwa kwa lengo la kufungua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo ya mijini na vijijini,” mwisho wa kunukuu.
Ilani hiyo inaeleza kuwa ili kufikia malengo kusudiwa yapo mambo kadhaa yatafanyika ikiwemo kuimarisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuongeza bajeti ili kukidhi mahitaji ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za vijijini na mijini.
Pia kuhakikisha kiwango cha barabara za changarawe kinaongezeka nchini kutoka kilometa 24,493 za sasa hadi kufikia kilometa 35,000 ifikapo mwaka 2025.
Vilevile kuongeza urefu wa barabara za mijini na vijijini zilizojengwa kwa kiwango cha lami kutoka kilometa 2,025 hadi kufikia kilometa 3,100 ifikapo mwaka 2025.
Kwa upande wa Mkoa wa Shinyanga ambako TARURA wanahudumia Halmashauri sita zilizoko kwenye mkoa huo kwa mwaka 2022/2023 TARURA ilipanga kufanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 675.3 kwa gharama ya zaidi ya milioni 700,fedha ambazo zimetoka Mfuko wa Barabara (Road Fund).
Meneja wa TARURA mkoani Shinyanga, Gilbert Mlekwa anasema kiasi cha milioni 300 ni miradi ya Jimbo,milioni 560 miradi ya tozo ya mafuta na milioni 400 ni miradi ya maendeleo Halmashauri ya Manispaa ya Kahama na jumla ya miradi yote ni zaidi ya bilioni 16.2.
Mlekwa anasema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2022, TARURA mkoani Shinyanga imefanikiwa kufanyia ukarabati mkubwa maeneo korofi ya barabara na kuwezesha kupitika hivi sasa kwa kipindi cha mwaka mzima bila shida.
Anasema kwa upande wa Manispaa ya Shinyanga wameweza kukarabati barabara za Bugweto – Ipeja umbali wa kilometa 5.2, Mohamed Trans – Dome – Ndembezi kilometa tano na Chibe – Ning’hwa umbali wa kilometa sita kwa zaidi ya milioni 501.6(501,636,400.00) na sasa barabara hizo zinapitika vizuri.
Anaendelea kueleza kuwa maeneo mengine korofi yaliyofanyiwa ukarabati ni Halmashauri ya Manispaa ya Kahama barabara ya Nyihogo – Ilindi kilometa 5.27 kwa shilingi 494,934,850.00, Ushetu, Ihata – Bugomba “B” Kanyanguli shilingi 486,798,220.00.
Kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ni barabara ya Nhobola – Mugunda kilometa 18 kwa gharama ya shilingi 487,455,000.00, Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Didia –Solwa kilometa 20 ambayo imegharimu shilingi 461,389,000.00.
“Kwa upande wa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama TARURA tumeweza kujenga kipande cha barabara ya Ilogi – Kakola namba tisa kwa kiwango cha lami umbali wa kilometa moja kwa gharama ya zaidi ya milioni 497″anasema Mlekwa.
Anasema katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 upande wa ufunguaji wa barabara za kuunganisha eneo moja kwenda eneo lingine TARURA katika Manispaa ya Kahama wamefungua barabara ya Nyihogo – Ilindi kilometa 5.27 kwa gharama ya zaidi ya milioni 494.
Halmashauri ya Ushetu barabara ya Ihata – Kanyanguli kwa kiasi cha zaidi ya milioni 486 huku kiasi cha zaidi ya milioni 487 kikitumika kwa ajili ya ufunguaji wa barabara ya Nhobola – Muguda kilometa 18 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.
Anasema kwa upande wa Madaraja na makalvati yaliyojengwa ndani ya kipindi cha miaka miwili – 2020/2021 na 2021/2022 na gharama zake ni mistari 153 ya Kalavati na madaraja mawili kwa jumla ya 2,054,120,000.
“Kwa kifupi yapo mafanikio kadhaa yameweza kupatikana ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuwawezesha wananchi kusafiri kwa uhakika kwa vipindi vyote vya msimu tofauti na zamani ambapo nyakati za masika baadhi ya maeneo mawasiliano ya barabara yalikuwa yakikatika,”anaeleza Mlekwa na kuongeza kuwa
“Kuuza mazao yao kwa bei nzuri maana masoko au wanunuaji wanafika kwa urahisi pia kuweza kufikia huduma za jamii kwa uhakika na vipindi vyote vya mwaka hali ambayo imewezesha kukuza uchumi wao ndani ya familia zinazowategemea,”.
Hata hivyo anasema TARURA katika kuhakikisha miundombinu inayotengenezwa ama kukarabatiwa inadumu kwa kipindi kirefu imekuwa ikitoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano ya viongozi pamoja na barua za maekelezo katika mbao za matangazo kwenye maeneo wanayoishi.
Meneja huyo wa TARURA anaendelea kueleza kuwa “Kwa mwaka ujao wa fedha tunatarajia kuendelea kufanya matengenezo,ujenzi wa barabara na madaraja kwa thamani zaidi ya bilioni 16 ambazo zinatoka kwenye mifuko mbalimbali ikiwemo tozo za barabara.”
Kwa upande wa fedha za tozo ya barabara TARURA mkoani Shinyanga inatarajia kupokea kiasi cha bilioni 5.5,kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali bilioni 3.5 na Mfuko wa Barabara kiasi cha bilioni 7.3 ambazo zote kwa pamoja zinaleta jumla ya zaidi ya bilioni 16.3.
Hata hivyo kila penye mafanikio daima hapakosi changamoto ambapo Mlekwa anasema baadhi ya changamoto zinazoikabili TARURA mkoani Shinyanga ni pamoja na uchache wa watumishi waliopo katika ofisi yake ikilinganishwa na majukumu yake.
Changamoto nyingine ni mgao mdogo wa fedha za matengenezo ya barabara ikilinganishwa na mtandao wa barabara,mahitaji pamoja na changamoto za dharura zinazojitokeza.
Ongezeko kubwa la ukuaji wa miji,biashara na migodi katika Halmashauri za Manispaa za Kahama na Shinyanga, kuongezeka kwa watu na magari ya uzito tofauti hivyo kuhitaji udhibiti wa uharibifu wa barabara hizo hususani za pembezoni zinazoelekea migodini mfano magari yenye uzito mkubwa wa mchanga wa madini.
Mafanikio ya TARURA yamepongezwa na wakazi kadhaa wa Mkoa wa Shinyanga hasa wale ambao hapo awali maeneo yao yalikuwa na changamoto ya miundombinu korofi ya barabara ikiwemo Kata ya Mwenge wilayani Shinyanga.
Diwani wa kata ya Mwenge, Edward Maganga anasema TARURA kwa kiasi kikubwa imewasaidia kutokana na kukarabati barabara muhimu inayounganisha kata yake na ile ya kwenda makao makuu ya wilaya hivyo wananchi wengi kuweza kusafiri na kufanya shughuli zao kwa uhakika.
“Miaka ya nyuma tulikuwa na changamoto sana kwenye kata hii kutokana na kutokuwa na barabara za uhakika hasa kuanzia pale njia panda ya Salawe kuja huku Kata ya Mwenge, tulilazimika kutembea umbali mrefu kuweza kupata usafiri wa kwenda wilayani kwa sasa kero hiyo haipo tena,” anaeleza Maganga.
Hata hivyo kwa upande wao baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu ambao ni wanachama wa kikundi cha Wachapakazi Gold Mine bado wanaiomba TARURA iwasaidie kukikarabati kipande cha barabara kutoka kijiji cha Nyandolwa hadi kwenye eneo lao la machimbo.
“Tunawaomba TARURA watusaidie sasa kututengeneza kipande hiki cha barabara kutoka pale kijijini Nyandolwa hadi hapa kwenye eneo letu la mgodi, maana tunapata tabu sana upande wa usafiri, wakumbuke sisi tunachangia kwa kiasi kikubwa pato la Serikali,” anaeleza Joshua Sayi Mwenyekiti Kikundi cha Wachapakazi Gold Mine.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika