Na Raphael Okello, Timesmajira Online,Mwanza.
MENEJA wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa Mwanza Mhandisi Ambrose Paschal amesema barabara ya Bulyang’hulu – Shibula inayojengwa kwa kiwango cha lami na kampuni ya kizalendo ya Mumangi Construction Ltd itakamilika Julai mwaka huu.
Amesema barabara hiyo ya mtaa wa Bulyang’ulu kwenda Shibula Kata ya Shibula Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ina urefu wa kilomita 2 na inatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.
Hayo yamebainishwa Machi 3,2024 katika maeneo tofauti kwenye Kata hiyo kufuatia zoezi la malipo kwa wananchi waliopitiwa na barabara hiyo katika makazi na mashamba jambo lililosababisha kuchelewa kuanza kwa kazi hiyo.
Mhandisi Ambrose amesema mvua nyingi zinazoendelea kunyesha imekuwa ni changamoto ya ucheleweshwaji wa kukamilika kwa barabara hiyo ambayo awali walimtaka Mkandarasi ajenge urefu wa kilomita 1.5 hata hivyo wakati akiendelea na kazi hiyo waliongeza nusu kilomita na kuwa Km 2.
Kwa upande wake Wakazi wa Kata ya Shibula wamefurahishwa na kampuni hiyo kuwashirikisha wazawa kwenye shughuli zake hivyo huchangia kufaidika na fedha ya serikali yao.
Baadhi ya wakazi hao wamedai kuwa kampuni nyingi za kigeni uajiri wataalamu wengi wa kigeni na kuacha wazawa jambo ambalo uchangia ukosefu wa ajira.
Diwani wa Kata ya Shibula Swila Dede ameshukuru uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kutekeleza wito wa kuwalipa fidia watu waliokuwa bado hawajalipwa kwani hawakuwa tayari kuanza ujenzi kwenye maeneo hayo bila fidia.
Ameipongeza pia kampuni ya Mumangi kwa kuwatumia vijana wengi toka eneo hilo katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa barabara hatua ambayo imepokelewa vizuri na wakazi wa mtaa huo.
Dede amefafanua kuwa kuwepo kwa hitaji la kampuni kurudisha sehemu ya fadhila kwa jamiii ni kitu cha kupongezwa ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa jamii husika.
Mkaazi wa Mtaa wa TX Mabuka Makingimika alishukuru namna Mkandarasi huyo alivyomwezesha kijana wake kupata kazi kwenye ujenzi wa barabara hiyo na kuanza kuwa na uzoefu wa kufanya shughuli hizo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba