September 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Barabara Buhongwa-Igoma,kufungua fursa za kiuchumi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Ujenzi wa barabara Buhongwa-Kishiri-Igoma, jijini Mwanza yenye urefu wa kilomita 14, umefikia asilimia 55, huku matarajio ya wananchi ni kufungua fursa za kiuchumi na huduma mbalimbali.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wananchi wa maeneo hayo, Septemba 25,2025,wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanislaus Mabula,ya kutembelea mradi huo kwa ajili ya kuangalia kasi ya utekelezaji wake.

Akizungumza na Timesmajira Online,Mkazi wa Kishiri,Mary Elia, ameeleza kuwa,wananchi wa maeneo hayo,kabla walikuwa wanapata shida ya usafiri hususani wajawazito kipindi cha kujifungua.Hata wafanyabiashara walikuwa wanapata shida ya kusafirisha bidhaa,hivyo uchumi ulikuwa chini.

“Barabara hii,ikikamilika tunatarajia uchumi kuongezeka,watu wengi watahamia huku ,matajiri watafanya uwekezaji katika maeneo yetu,wananchi tutapata huduma vizuri na biashara zitaenda vizuri,wanawake wanajifungua vizuri kwa sababu usafiri utapatikana kwa haraka.Tunaomba mradi ukamilike kwa wakati ili tupate huduma kwa unafuu na kwa uharaka zaidi, kama wengine wanavyopata,”amesema Mary.

Joyce Mathias,amesema walikuwa wanapata changamoto ya kutumia muda mrefu kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine,akitolea mfano kutoka Kishiri hadi Igoma,iliwachukua takribani saa moja kufika eneo hilo.”Barabara hii ikikamilika,itatuondolea vumbi,ambalo limetutesa kwa muda mrefu,itafanya maeneo haya kuwa mjini na wenye maduka kiwango cha kufanyabiashara kutaongezeka,”amesema Joyce.

Mkazi wa Igoma,Moses Manassa, amesema matarajio yao,kupitia barabara hiyo,maisha ya wananchi yataboreshwa na kutoa fursa nyingi hususani wa biashara kwani kutakuwa na muingiliano wa watu na mpaka kwa mpaka.

“Serikali ijaribu kuangalia watu,na itende haki katika utekelezaji wa miradi, ili wanaostahili kulipwa fidia walipwe kwa wakati na iwe inafuatilia,ili kubaini migogoro iliopo,”.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, Stanislaus Mabula,amesema,barabara hiyo itakuwa na tija,kwanza itaufungua Mji wa Mwanza,na italeta fursa nyingi,kwani inatokea Buhongwa kuja Igoma.Ni njia rahisi yakumtoa mwananchi alitefika Buhongwa kwenda Kisesa,kuliko ile ya kupitia Usagara moja kwa moja.

“Kuna fursa za kibiashara,mazao yote yanayotoka Wilaya za Kwimba, Misungwi,vijijini wanaleta mjini kwa sababu wanaamini kuna biashara.Hivyo itakuwa fursa kwao na kwa wafanyabiashara wa kwetu, kwa sababu watapata bidhaa kwa muda mfupi kwa gharama nafuu, ukilinganisha na kuzunguka mjini mpaka hapa.Barabara hii itakuwa na taa karibia 400,ukiamua kufanya matembezi unaweza kutembea bila wasiwasi Buhongwa hadi Igoma,”amesema Mabula na kuongeza:

“Wanatarajiwa kuwa na vituo 24, vya daladala,kwa barabara nzima upande wa kulia na kushoto,hivyo tunaamini yale maeneo ambayo yanamsongamano wa watu,kama ya biashara,soko na huduma za kijamii,yapewe vipaumbele kwenye vile vituo,ili yaweze kusaidia watu kupanda na kushuka kwa wakati mmoja, na tutakuwa tumeutendea haki mradi,”.

Hivyo ametoa wito kwa wananchi, mradi ukikamilika kila mtu awe mlinzi kwani kutakuwa na miundombinu ya taa,vituo bora vya daladala,njia za watembea kwa miguu,watunze na kulinda ili iwe na tija wakati wote.

Mratibu wa mradi wa barabara Buhongwa-Kishiri-Igoma ,Mhandisi wa Jiji la Mwanza,Ukelewe Tungaraza,amesema mradi huo, umegharimu kiasi cha bilioni 22.7,ulianza Novemba 20,2023.Mkandarasi anatakiwa kukabidhi mradi ukiwa umekamilika Februari 19,2025.

“Mpaka sasa, Mkandarasi amekuwa akishughulika kutengeneza tuta la barabara,ambapo barabara kutoka Buhongwa hadi Igoma Center,yameguswa,na sasa anamalizia daraja na sehemu chache ya kuhakikisha lile tuta linakamilika.Kazi za kujenga matabaka ya barabara itaanza Oktoba,2024, atakwenda nayo kwa kasi kwa sababu tayari barabara itakuwa imeisha onekana,”amesema Mhandisi Tungaraza.