Na Philemon Muhanuzi, Times Majira Online, Dar es Salaam
NIMEFURAHISHWA kuona msimu huu wa matangazo ya biashara pale Kilwa Road Sabasaba klabu ya Yanga imeamua kutoka kidigitali zaidi.
Ni wazo jema sana na haswa yule muasisi wake ameiona fursa ambayo wenye dhamana wengi tu pale Yanga hawakuwa wakiiona miaka ya nyuma.
Yanga ilikuwa imehodhiwa na aina ya mawazo yasiyotaka kwenda na ukweli wa wakati husika. Ilikuwa ni taasisi yenye wanachama wanaoridhika kufanya mikutano katika kumbi mbalimbali na kuchagua viongozi halafu jipya linakuwa halionekani.
Wanachama wanaopewa uongozi wakawa wanaridhishwa na ule umaarufu wa picha zao kupamba kurasa za michezo.
Siku zinakwenda na wale waliowachagua wakishaanza kuwachoka, wanatengeneza mazingira ya kuandaa mkutano mkuu ili waingie wengine wapya ambao labda watakuja na akili mpya.
Huo ndio ukawa mzunguko wa maisha ya Yanga. Wengine wakiona ufahari kushinda ndani ya ukumbi wa klabuni huku wakicheza karata kutwa nzima.
Sifa ya wanachama wa aina hiyo ikawa ni kumfungia kocha mlango ili asiingie klabuni baada ya kupewa timu na kushindwa kuleta matokeo mazuri.
Leo hii unaporushiwa video jongevu yenye kuelezea kuhusu banda lao maalum pale uwanja wa maonyesho ya biashara maarufu kama Sabasaba, unagundua uwepo wa fikra zenye kutaka kuipeleka Yanga mbali kwenye ulimwengu halisi wa kisasa. Ni mawazo mazuri sana.
Wapo watoto wa mashule ya msingi ambao wanaiona Yanga magazetini, wanapokwenda katika banda la klabu wanaitambua kwa ukaribu zaidi. Wanapopiga picha pembeni ya makombe wanakuwa wamepata timu mpya ya kushabikia.
Haitoshi tu kwa wale wanachama na mashabiki wenye umri mkubwa kujivunia jina na hadhi ya klabu pasipo kuwepo jitihada za klabu yenyewe kuendelea kuishi ndani ya fikra, malengo na mipango ya watu wa vizazi vipya.
Natoa ushauri kwa viongozi wa Yanga katika kipindi hiki cha maonyesho ya Sabasaba, ipo haja na sababu ya msingi ya kuongea vizuri na wachezaji wao wa zamani waliotamba miaka ile ya 1970,80 na 90.
Ni jambo la maana kama Sunday Manara akiwepo bandani ili hawa wanayanga watarajiwa waweze kumjua vizuri kwa kumuona kwa karibu.
Ipo haja kwa Omari Hussein kuwepo pale bandani ili aweze kuelezea historia kwa kijana ambaye alikuwa bado hajazaliwa miaka ile ya 1980 mwanzoni.
Ipo sababu muhimu kabisa kwa wachezaji wengi wa zamani waliofanya makubwa wakiichezea Yanga, kuwepo katika maeneo ya banda la timu.
Tshishimbi ni kiongozi mzuri na amependwa na wanachama pamoja na mashabiki wa kizazi cha sasa. Lakini wapo wanasoka wa zamani waliotengeneza heshima inayojivunia klabu kwa sasa.
Hawa sehemu yao ni pale Sabasaba, klabu iangalie namna ya kuwalipa kwani na yenyewe inao uhakika wa kujitangaza. Ni biashara yenye faida za pande mbili, upande wa klabu na upande wa wanasoka wa zamani.
Haitoshi kulipamba banda kwa kuyapamba vizuri makombe ili waingiaji wapige picha za kumbukumbu halafu uwe ndio mwisho wa kila kitu. Yanga ifikirie juu ya uwezekano wa kuanda DVD zenye historia ya klabu.
Uwepo mkusanyiko wa video za mechi zote zinazoweza kupatikana. Siku zote historia ya zamani inayotunzwa vyema ndio inayoweza kuiuza klabu.
Banda la Yanga Sabasaba ni sehemu inayoweza kuwa ni mwanzo wa mahusiano mapya kati ya mwanayanga mpya na klabu inayozidi kuwa na umri mkubwa. Wapo wanayanga wapya wengi tu miongoni mwa wanaoingia ndani ya banda la klabu pale Sabasaba.
Hawa ni vijana wasiozifahamu zile siasa za mikutano mikuu yenye nia ya kuwatoa viongozi madarakani. Ni kizazi cha vijana wenye kumiliki Iphone za shilingi milioni moja, kinategemea kuiona Yanga ikifanana na timu za Ulaya.
Hawa na wanayanga wenye kila sababu ya kuijua historia ya klabu kutoka kwa wanasoka walioiweka hai historia hiyo ambao bado Mwenyezi Mungu anaendelea kuwajalia pumzi.
Wakiingia ndani ya banda na wazione picha za mechi ya Yanga na Simba ya mwaka 1974 na wapate maelezo ya kweli. Wakiendelea kutazama makombe na wazione picha za Yanga na El Merreikh mwaka 1986, na wapewe maelezo mazuri.
Yanga inapoweza kuwa na banda la kujitangaza na lisiishie kujaa biashara peke yake, historia ya timu inayotangazwa vyema na kueleweka kila inapoelezewa huwa ni chanzo cha maelfu ya mashabiki wapya.
Hongera maalum zimfikie yoyote aliyeanzisha wazo la Yanga kuwa na banda lake pale Sabasaba unapofika msimu wa maonyesho ya biashara.
More Stories
Naibu Waziri wa Fedha abariki ujio mpya wa Bahati Nasibu
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes