November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balile: Vyombo vya habari vinadai taasisi za kiserikali zaidi ya Bil. 7.8

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Imeelezwa kuwa, vyombo vya habari binafsi, mpaka sasa vinadai taasisi za serikali pesa za matangazo zaidi ya Tsh. 7.8 Bil. Taasisi hizo zinakwepa kulipa.

Pesa hizi ni nyingi, na kutolipwa katika vyumba vya Habari, kumesababisha kuyumba, hili ni moja ya jambo muhimu katika mapendekezo yetu ya mabadiliko ya sheria za habari tunakwenda kuzungumzia.

Ni kauli ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akizungumza na Abdallah Kurwa katika Kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One leo.

Balile amesema, taasisi za serikali zinadaiwa pesa nyingi na vyombo vya habari lakini hawalipi, hivyo kuundwa kwa sheria kwamba wasipolipa watafungwa, itaongeza msukumo.

“Tarehe 11 na 12 Agosti 2022 katika mkutano wa wadau wa habari, hatuendi kushikana mashati na serikali bali tunakwenda kupigania maslahi ya wanahabari na vyoimbo vyao.”

“Vyombo vya Habari binafsi vinadai taasisi za serikali zaidi ya Tsh. 7.8 Bilion na hawalipi kwa kuwa hajkuna msukumo wa kufanya hivyo, moja ya msukumo wa mabadiliko hayo ni kuweka sheria ya kuwafunga pale watakaposhindwa kulipa,” amesema mwenyekiti huyo.

Kiongozi huyo wa TEF amesema, vyombo vya habari kama ilivyo uwekezaji katika maeneo mengine, vinahitaji mtaji na biashara kubwa ni matangazo.

“Wanaposhindwa kulipa matangazo, maana yake wanasababisha shida kwenye vyombo vya Habari maana ili viendeshwe vinahitaji fedha, Bilioni 7.8 ni nyingi sana.”

“Hapo kuna mishahara ya waaandishi, wafanyakazi wa sekta zingine kwenye vyombo vya habari, kuna fedha za uchapaji lakini pia matumizi ya ofisi, fedha hizi zisipolipwa ofisi zitaendeshwaje?,” amesema Balile.

Amesema, jambo hilo alimueleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kutoa maelekezo kwa taasisi za serikali kulipa madeni hayo, pamoja na maelezo ya Waziri Mkuu, taasisi za serrikali hazijatekeleza.

“Jambo hili nililifikisha kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu akatoa maelezo kwa taasisi husika zilipe fedha za matangazo, lakini wengi wao mpaka sasa hawajalipa.”

“Sasa kwenye mkutano huo, mambo kama haya tutazungumzia na ndio maana tunataka kuwe na sheria za namna hii, ili kulinda maslahi ya waandishi na uhai wa vyombo vya habari nchini,” amesema Balile.

Amesema, wanahabari wamekuwa wakiwajibika kwa namna utaratibu unavyoelekeza na ndio maana vyombo vya Habari vinatumika kupeperusha matangazo, lakini wajibu wa baadhi ya taasisi hautekelezwi.

“Sasa katika mabadiliko haya, suala la malipo ya matangazo liwekwe kisheria, atakayekaidi ajue kwamba ipo sheria na atawajibika kwayo,” amesema Balile.

Pia Balile amesema, TEF na wadau wa Habari wanasisitiza uhuru wa vyombo vya Habari katika kujisimamia kama ilivyo tasnia nyingine nchini.

“Unajua sijui kwanini tasnia ya habari inawekwa mikono, nakumbuka wakati ule wa Mkutano wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka huu, walimu waliytaka kuandamana, serikali ikwenda mahakamani usiku kuomba zuio. Kwanini heshima hiyo isiwe kwenye tasnia ya habari pia.”

“Yaani huku Mkurugenzi wa Habari anakuwa mlalamikaji, msikilizaji na hakimu, hapo huwezi kutenewa haki. Tunataka kuwepo na Baraza Huru la Vyombo vya Habari ambalo serikali ikiwa na jambo lake ama imekwazwa iende huko, sio wao ndio walalamike, wasikilize na kuhukumu,” amesema.