Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
Hayo ameyasema Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, wakati akizungumza katika Kipindi cha Mezani kinachorushwa na Kituo cha Redio cha EFM, leo jijini Dar es Salaam.
Akieleza nafasi ya mwandishi wa habari kwenye jamii Balile amesema, kwa sasa kila mmoja anaweza kutoa taarifa ama kupiga picha lakini kazi ya mwanahabari ni zaidi ya kupiga picha na kutoa taarifa pekee.
“Kila mtu anadhani akijua kusoma na kuandika anaweza kuwa mwandishi, hapana. Tunasema, kila kipaji lazima kiendelezwe. Taaluma ya Habari ina maadili na hapo ndio tofauti inapoonekana,” amesema.
Balile amesema siyo kila mtu anayejua kusoma na kuandika anaweza kuwa mwandishi wa habari, bali lazima kipaji kiendelezwe kwani uandishi una kanuni na miiko yake.
Akizungumzia mabadiliko ya sheria za habari amesema, sheria ikitungwa ili kudhibiti habari, huwa na matatizo yaliyojificha, lakini ikiwa ni wezeshi, hutoa fursa ya kupata mawazo mapya yanayolenga ufanisi zaidi.
“Unapotunga sheria ya kuzuia ama kuminya habari, ujue kuna madhara makuba unayatengeneza hapo mbele. Ndio maana tunazungumza na serikali ili tuwe na sheria zinazokubalika kimataifa.
“Tusifurahie kutunga sheria mbaya kwa ajili ya kuumiza wengine, tusitunge sheria kwa ajili ya kukomoa waandishi bali tutafute ufanisi katika tasnia ya habari,” amesema.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote