December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balile: Kuna matumaini kwenye Bunge la Septemba mwaka huu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile amesema kuna matumaini kwenye Bunge la Septemba mwaka huu, mapendekezo ya mabadiliko ya sheria za habari, yakasomwa kwa mara ya kwanza.Balile ameyasema hayo jijini Dar es Salaam akizungumzia wito wa serikali kukutana na wadau wa habari nchini.

Hivi karibuni, serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeitisha mkutano wa wadau wa habari kuzungumzia vipengele mbalimbali vya habari vinavyoonekana kuminya tasnia hiyo.

Taasisi 10 zimeandikiwa wito wa kuhudhuria mjadala huo, mjadala huo utahusu mabadiliko ya vifungu mbalimbali vya habari ambayo wadau wanapiga kelele kwamba, vinaminya uhuru wa habari nchini.

Balile amesema, mchakato umeanza kuzaa matunda.

“wiki hii tumepata mwaliko kutoka serikalini ambapo tutakuwa na mkutano wa pamoja kati ya serikali na wadau wa habari utakaofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere.”

“Kuna mwelekeo sasa kwamba, kama tunakwenda kwenye huu mkutano wa tarehe 11 na 12 Agosti mwaka huu, tunaweza kuona hii sheria inapelekwa bungeni Septemba mwaka huu kwa ajili ya kusomwa kwa mara ya kwanza.”

“Sasa tusiende kusoma sheria ambayo kwamba tutaenda na mivutano, tumeishakubaliana na Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye, tumeishakubaliana na mheshimiwa rais (Rais Samia Suluhu Hassan), kwa hiyo tunaamini kwamba, watatusikiliza kwenye mkutano na tutalizungumza ili tupitie yote ili tusipeleke vipande vipande.”

Amesema, mjadala huo unahusu kujadili vifungu vya sheria za habari ili kuona jinsi gani tunarekebisha kifungu kwa kifungu, ili ziwe nzuri kama wadau walivyoomba.

Amesema, mchakato wa mabadiliko umepiga hatua kubwa tangu ulipoanza na kwamba, hatua ya serikali kuitisha mkutano wa wadau kujadili vipengele vya sheria hizo, unaashiria kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuwasilishwa kwenye Bunge la Septemba mwaka huu.

Balile amesema, kwenye mapendekezo yao miongoni mwa vipengele wanavyotaka kufanyiwa kazi ili kulinda uhuru wa habari ni pamoja na kuondoa utitiri wa vyombo vinavyosimamia tasnia ya habari.Na kwamba, muundo wa vyombo vilivyoelekezwa na sheria iliyopo, unaweza kuvunjwa na kuunda chombo kimoja ambacho kitakuwa imara na kusimamiwa kisheri kama ilivyo katika taaluma nyingine nchini.

“Sisi hatupingi Bodi ya Ithibati ila tunasema kwamba, kutenga Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Vyombo vya Habari, unakuwa umeleta shida kwasababu, ukiwa na Baraza la Ithibati halafu Baraza Huru la Habari, unakuwa na vyombo viwili vinavyofanya kazi ile ile.

“Lakini tunasema, kama wanasheria wanayo Tanganyika Laws Society; Hiyo hiyo inafanya kazi ya ithibati (inawapa vitambulisho), inasuluhisha pale mwanasheria anapokwenda kinyume. Hivyo, tunataka chombo kimoja (Baraza la Habari) litakaloundwa kwa mujibu wa sheria liwe na mamlaka yote hayo,” amesema Balile na kuongeza;

“Baraza tunalotaka litakuwa na kazi ya kufanya ithibati; kwamba litawapa waandishi vitambuliisho, litashughulikia kesi zinazohusu tasnia ya habari lakini kama ilivyo sasa.”

Amehoji, ikiwa taaluma nyingine kama madaktari, wagavi pia mainjinia wamekuwa na bodi zao ambazo zinashughulikia kila kitu kinachowahusu, lakini kwenye tasnia ya habari igawanywe vipande vipande.

Amesema, kuna vipengele vingi ambavyo vinapaswa kuguswa kwenye maboresho hayo, hata hivyo ameisifu serikali kwa hatua ya kukutana na wadau ili kuingia katika hatua nyingine ya mabadiliko ya sheria kandamizi za habari nchini.