January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BAKWATA:Puuzeni uzushi wa Kigogo huko Twitter,vyuo, ibada kama awali rasmi

Na Irene Clemence
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetagaza kufuguliwa kwa  baadhi wa vyuo vya dini na shughuli nyingine za ibada za jumuia kuendelea kama awali.

Msemaji wa Mufti ,ambaye ni Katibu wa Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Hassan Chizenga amesema, kufunguliwa vyuo akutahusisha madrasa ya watoto wadogo na kuwataka kuendelea kusubiri hadi Serikali itakapotoa maelekezo.

Sheikhe Chizenga anasema,  pia mikusanyiko ya kidini na kiibada nje ya nyumba za ibada kama vile kwenye kumbi na mfano wa hizo zitakazowahusu watu wazima ziendelee kwa kufuata taratibu za afya zilizowekwa.

Amesema, ruhusa hiyo imetolewa pamoja na kuzingatia kuchukua tahadhari zote za kiafya kama vile kunawa mikono kwa maji tiririka.

Pia amesema, BAKWATA inamshukuru Mungu kwa kuwapatia watanzania Rais mwenye hofu ya Mungu na mwenye maono ya kiimani na ya kishujaa ya kutangaza wazi kuwa Mungu ndio silaha namba moja ya kupambana na COVID-19.

Katika hatua nyingine BAKWATA limekanusha uzushi katika mitandao ya kijamii kwa lengo la kuvuruga jamii ya Kiislamu.

“Kuibeza dini yetu na kuvunja umoja uliojengwa na Mufti  wetu akishirikiana na viongozi wengine ni uadui mkubwa,”amesema Chizenga.


Amesema,  kuna baadhi ya watu wanatumia akaunti ya Twitter ya Kigogo ambao wamezusha uongo wenye chokochoko kuwa maafisa usalama wa wilaya wameagizwa kujua idadi ya msikiti yote kila wilaya na mashekhe wa wilaya wamepewa jukumu hilo.

“Tunakanusha habari hizi za uongo na uzushi zinazotaka kuwavuruga waislamu kwa lengo la kuvunja umoja uliopo sasa”anasema Chizenga.


Shekhe Chizenga aliwataka watanzania kutowasikiliza watu kama hao ambao wanataka kuwapotoshwa waislamu wengine kwa kutumia mitandao ya kijamii.

“Nawazindua watanzania na waumini wa dini zote kuwa watumiaji wa akaunti ya kigogo ni maadui wakubwa wa imani yeyote na wasimpe nafasi mioyoni mwao hata kidogo,”amesema Chizenga.