Na.Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ukerewe,Ally Mambile,kwa niaba ya Katibu wa CCM mkoani Mwanza,Omari Mtuwa, leo amezindua safari za Hija mwakani na kuwataka Waislamu kujiandaa kiuchumi ili kutimiza nguzo hiyo miongoni mwa tano za Uislamu.
Mambile amesema muumini wa Dini ya Kiislamu anayetaka kwenda kuhiji sharti awe na nguvu na uwezo kiuchumi,hivyo ni busara kuwaandaa waislamu mapema ili wakatekeleze ibada hiyo.
Amesema nguzo mbili (zaka na hija)zinahitaji uchumi na siku zote mtu hawezi kufikia mafanikio uchumi hadi awe ametekeleza mambo mawili,la kwanza awe na nguvu na jambo la pili ni nauli,hivyo waislamu watofautishe hadhara hiyo na zingine,waitumie kuhamasisha watu wakahiji.
“Ni hadhara kubwa ya kuwaandaa waislamu kutekeleza ibada ya Hija iliyo miongoni mwa nguzo tano za Uislamu,kwa kiasi kikubwa zote zinategemeana.Huwezi kuwa mwislamu kwa kufunga,kutoa zaka,shahada na swala ya Ramadhani bila Hija,lazima uhakikishe unatimiza nguzo hizo,”amesema Mambile.
Ameeleza kuwa viongozi wana jukumu la kuwandaa waumini ili kupata waislamu wazuri wenye mioyo iliyojaa imani thabiti watakaoweza kutoa fedha kati ya sh.milioni 14 hadi milioni 15 kwenda kuhiji kwani kutoa fedha hizo kunahitaji moyo na imani iliyojikita sawa sawa.
“Rai yangu kwa vijana,anayefahamu ni Mcha Mungu aanze kujiandaa mapema kwa kuhifadhi fedha anazopata awe na uwezo wa kiuchumi na ipo siku atakuwa ni miongoni mwa mahujaji,ili kufanya ibada ya hija njema kwa hili nitaomba matokeo ya uzinduzi huu,” amesema Mambile .
Ameeleza yanayoyafanywa ya ulimwengu na wenye uwezo yasikitisha sana, wananunua moto kwa gharama kubwa badala ya pepo kwa gharama ndogo na kufanya mashindano ya kubadilisha magari ya kifahari kwa fedha wanazokusanya ambapo mtu yuko radhi kununua gari la milioni 200 akamhonga mwanamke.
Mwenyekiti huyo wa CCM amesema kazi kubwa anayoifanya Sheikhe Hasani Kabeke ya kumuunga mkono Mufti anatarajia ilete athari na matokeo chanya, hivyo waislamu waachane na yasiyo na matokeo,kipengele ambacho wamekisahau na kila wanalofanya lazima watarajie matokeo.
Mambile kwa niaba ya CCM Mkoa aliishukuru BAKWATA kuona umuhimu wa kuwaalika viongozi wa CCM kuzindua safari za hija kupitia taasisi hiyo, binafsi amefarijika kuandika historia na kumpongeza Sheikh Kabeke (Sheikhe wa Mkoa)kuwa,baada ya kupata dhamana ya uongozi mafanikio ya harakati za maendeleo ya uislamu yanaonekana.
Kwa upande wake Alhaji Sheikhe Kabeke amesema kuitumia BAKWATA kwenda hija kuna manufaa makubwa,ni taasisi pekee yenye uzoefu wa kuwasafirisha mahujaji tangu mwaka 1969,hivyo waislamu wajitokeze kwa wingi kujisajili kwenda katika ibada hiyo yenye faida nyingi.
“Tunawahamasisha waislamu watumie fursa ya uzinduzi wa safari za hija kujisajili ikiwezekana kila wilaya ipeleke hujaji mmoja na kuna raha kwenda hija ukiwa na nguvu pia Idara ya Tahiwid na Dawa ihamasishe watu wakahiji,wapite katika njia salama (BAKWATA)kwani ukienda hija unakuwa mgeni ya Mwenyezi Mungu na uwapo Makka na Madina unakuwa mgeni wa Mtume Muhhamad S.A.w,”amesema.
Naye Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Chanila amesema gharama za usafiri wa kwenda na kurudi zikiwemo huduma muhimu za kijamii ni Dola za Marekani 6000 kwa hujaji mwenye hati ya kusafiria atakayejisajili kupitia baraza kuu hilo la waislamu,kabla watatakiwa kupata chanjo ya Uviko-19 na kupata cheti.
Awali Mkurugenzi wa Hija BAKWATA Makao Makuu,Haidari Kambwili amempongeza Sheikhe Kabeke kwa kutekeleza maelekezo ya Mufti na kuzindua safari za hija mapema kutokana na mabadiliko na kuhimiza watu kujisajili ili kuondoa changamoto ya kushindwa kwenda kuhiji Juni 26,mwakani.
More Stories
Jela miezi sita kwa kuvaa sare za JWTZ
Watolewa hofu uvumi juu ya uwepo wa Teleza
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini