April 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BAKWATA yawazawadia washindi wakuhifadhi Qur’an

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

KATIKA juhudi za kulea kizazi chenye maadili na hofu ya Mungu, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,limewazawadia vijana walioshiriki mashindano ya kuhifadhi Qur’an zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitungi ya gesi na fedha taslimu.

Washindi sita wa mashindano hayo walipewa zawadi hizo,huku washiriki wengine 12 wakituzwa pia kama njia ya kuwahamasisha na kutambua juhudi zao za kuipenda na kuihifadhi Qur’an tukufu.

Lengo kuu la mashindano hayo ni kuwajengea vijana uwezo wa kuielewa Qur’an,kuipenda na kuihifadhi, sambamba na kuwalea katika maadili mema na maisha ya uadilifu.

Watoto wanaofundishwa Qur’an wanajengwa kuwa raia wema, waaminifu na wenye hofu ya Mungu hata wanapopata ajira au madaraka.

 Kwa mujibu wa Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke , amesema zawadi  ya mitungi ya gesi  ni  ya kihistoria na mkakati wa kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, na badala yake kutumia nishati safi kama gesi, ili kulinda mazingira na kupunguza uchafuzi wa hewa ukaa.

“Tunahamasisha utunzaji wa mazingira kama sehemu ya mafundisho ya Qur’an. Kupika kwa kuni na mkaa kunaharibu mazingira. Hii ni njia ya kushiriki kwa vitendo katika kulinda dunia yetu,” amesema Sheikh Kabeke.

Aidha, ameeleza kuwa mitungi hiyo ya gesi imetolewa kupitia msaada wa Zakaria Nzuki, ambaye amekuwa akiunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na hewa ukaa,hadi sasa zaidi ya mitungi 70 imetolewa kwa jamii mbalimbali.

Pia amesema katika kuongeza hamasa na uelewa wa watoto kuhusu utalii wa ndani,  aliwaahidi washindi hao safari ya kutembelea Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane ili kujifunza kuhusu wanyama na vivutio vya asili vya Tanzania.

Haya hivyo amesema Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally Mbwana amekuwa akihimiza utunzaji wa mazingira kwa kuhimiza upandaji miti nchini kote, hivyo BAKWATA Mwanza imefanya  kwa vitendo kwa kuweka mkakati wa kupanda miti kila wilaya ili kulinda mazingira na kutekeleza mafunzo ya dini kwa vitendo.

Katibu wa Umoja wa Walimu wa Madrasa (UWAMA) Mkoa wa Mwanza, Amani  Ibrahim amesema utoaji wa zawadi hizo ni kutimiza ahadi kwa washindi na ni fursa ya kuonesha fadhila kwa jamii ya Kiislamu.

“Mikakati yetu tunawafundisha watoto si tu kuhifadhi Qur’an bali pia kuwalea na kuwajenga katika maadili mema wawe na hofu ya Mungu. Tunaamini Qur’an inawajenga watoto kuwa na misingi imara ya maisha”.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha BAKWATA Online, Musabila Raphael, amesisitiza kuwa zawadi hizo ni kichocheo kwa watoto kupenda Qur’an na kuielekeza katika maisha yao.

“Kumlea mtoto na kumpa mapenzi ya Qur’an kutamfanya awe raia mwema,ni njia bora ya kupandikiza maadili ya uadilifu na hofu ya Mungu mapema,” amesema Raphael.

Pia amepongeza Umoja wa Walimu wa Madrasa kwa kuandaa mashindano hayo na kuhimiza mikoa mingine kuiga mfano huo ili kujenga taifa lenye misingi ya imani, maadili na uzalendo wa kweli.