January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BAKWATA waomba somo la dini liingizwe kwenye mitaala

Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,limeiomba Serikali kuingiza somo la dini kwenye mitaala ya elimu ili kuwafanya watoto wawe na hofu ya Mungu.

Hiyo ikiwa ni njia ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili huku Chama Cha Mapinduzi (CCM),kikipendekeza wanaolawiti watoto wakatwe sehemu ya viungo vyao.

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu (hawapo pichani) wakti wa futari iliyoandaliwa leo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara,Omari Christopher Gachuma,leo jijini humu.

Pia BAKWATA imempongeza mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC)Mkoa wa Mara,Christopher Gachuma kwa kuwakutanisha na kuwafuturisha waislamu kwa miaka 28 licha ya kuwa imani tofauti ya dini.

Hayo yalielezwa jijini Mwanza,leo jioni kwa nyakati tofauti na viongozi wa dini,chama na serikali wakati wa futari iliyoandaliwa na Gachuma kwa ajili ya waumini wa dini ya Kiislamu kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hassan Kabeke,amesema viongozi wa dini na jamii wanahangaika kusaka suluhu ya mmomonyko wa maadili ili kujenga nchi ya watu waadilifu. Hivyo serikali iangalie namna ya kuingiza somo la dini kwenye mitaala watoto wapate elimu ya dini wakiwa wadogo kwani kwa sasa hofu ya Mungu haipo.

“Tunahangaika na maadili yamekuwa tatizo na mambo yameshaharibika,watoto hawasomi elimu ya dini hawana hofu ya Mungu……,tumesikia serikali kuhusu mmomonyoko wa maadili na vitendo vya ushoga,tunaipongeza kwa kufuta vitabu vilivyoingiza mambo mabaya kwenye mitaala na kupiga marufuku watoto wa umri chini ya miaka 10 wasipelekwe shule za bweni,” amesema Sheikhe Kabeke.

Amesema kwenye vitendo vya ushoga serikali imeonesha msimamo kupitia kwa Makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiagiza vyombo vya dola viingie ndani kuchunguza na kudhihiti jambo hilo na kuwataka waislamu kumwombea Rais Samia kwa suala la mmomonyoko wa maadili na chama kinachotawala.

Sheikhe huyo wa mkoa ametumia fursa hiyo kumpongeza Gachuma kuwafururisha waislamu na wasio waislamu jijini Mwanza kwa miaka 28,anatoa mwanga kwa wengine wenye uwezo na si kujionesha bali liko ndani ya nafsi yake na amebeba mengi ya uislamu kwani kutoa ni moyo.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Begga,amesema suala la mmomonyoko wa maadili atalifikisha kwenye Chama ili liingizwe kwenye ilani ya uchaguzi iwe rahisi kutekelezwa na viongozi huku akipendekeza watu wanaowalawiti watoto itungwe sheria ili wakithibitika wakatwe kipande cha maumbile yao kupunguza ama kukomesha vitendo hivyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassani Masala,kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima,akizungumza na waislamu (hawapo pichani) leo baada ya kumaliza kufuturu,chakula kilichoandaliwa na Mjumbe wa NEC Mkoa wa Mara,Omari Christopher Gachuma.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika futari hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Adam Malima,amesema Sheikh Kabeke ana uhusiano mzuri na serikali,bila hivyo anaamini fursa nyingi wasingezipata.Hivyo amewataka waislamu kutunza na kudumisha amani huku akimshukuru Gachuma kwa upendo wa kuandaa na kushiriki ibada iliowakutanisha wengi na amekuwa mshiriki wa maendeleo ya mkoa,chama na Serikali.

“Sheikh Kabeke,mambo unayotenda kwenye jamii Mwanza umeweza kusaidia kuyatatua na hili la maadili kuna umuhimu wa kuhuisha mitaala yetu,kuna vitu hatukufanya vizuri na ni wajibu wa serikali kuyaona na kuyaingiza yaliyo bora kwenye mitaala ili kujenga kizazi cha maadili bora,”amesema Masala.

Naye Gachuma amesema anafarijika kuona waislamu wakiitikia mwaliko wake,anafahamu faida za uislamu ni nyingi na hivyo ataendelea kufuturisha hadi mwisho wa wa uhai wake duniani.Pia marafiki zake wengi wakiwa waislamu kuliko wakristo,hana njia ya kutoka kwenye uhusiano huo na ataendelea kuyadumisha aliyoyaanzisha.

Mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa na Mjumbe wa NEC Mkoa wa Mara,Omari Christopher Gachuma,akitoa nasaha zake kwa waumini wa dini ya Kiislamu (hawapo pichani) baada ya kumaliza kufuturu, futari aliyoiandaa leo jijini Mwanza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Juma Chikoka, amesema anayoyafanya Gachuma kwa waislamu ni uwekezaji wa dhati katika mioyo ya watu kwani hawangalii miaka mingapi uliyoishi duniani bali ulifanya nini kilicho alama katika mioyo yao na kuahidi kuiga na kuiga si vibaya.

Akizungumzia mmomonyoko wa maadili,amewaasa waislamu na Watanzania kuendelea kuheshimu mila,desturi na utamaduni wetu pia mataifa meingine yanayokumbatia hayo yaziheshimu mila zetu na kwamba wilayani Rorya amewatahadharisha atakayebainika kufanya vitendo hivyo sheria zipo zitachukua mkondo wake.

Waumini wa dini ya Kiislamu, wakiwasikiliza baada ya viongozi wa dini, Chama na Serikali,baada ya kufuturu leo,futari iliyoandaliwa jijini Mwanza na Mjumbe wa NEC wa Mkoa wa Mara, Christopher Gachuma.