December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BAKWATA Tabora wampongeza Rais Samia

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoani Tabora limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwaletea maendeleo Watanzania.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Shehe Mkuu wa Mkoa huo Shehe Ibrahimu Mavumbi alipokuwa akitoa salamu katika Hafla ya Baraza la Idd iliyofanyika jana katika ukumbi wa Chuo Cha Utumishi Umma (TPSC) Mkoani hapa.

Amesema kuwa katika miaka 3 ya utawala wake Rais Samia amefanya kazi nzuri sana ya kuwaletea maendeleo wananchi na kusimamia kwa moyo wa dhati umoja na mshikamano wa Watanzania wote pasipo kujali itikadi zao za kisiasa au dini.

‘Tunampongeza sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake mzuri na kuendelea kuunganisha Watanzania wote kuwa kitu kimoja, hili limekuwa chachu kubwa ya kuendelea kudumishwa amani na utulivu wa Watanzania’, amesema.

Shehe Mavumbi ameomba waumini wote wa dini hiyo na jamii kwa ujumla kuendelea kumwombea dua njema ili Mwenyezi Mungu amwongoze katika majukumu yake na kumfanyia wepesi katika kila jambo.

Amemhakikishia kuwa Mashehe wa Mkoa huo na waumini wote wa dini ya kiislamu wataendelea kuunga mkono juhudi zake ikiwemo kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya jamii.

Aidha amewataka waumini wa dini hiyo kuendeleza mazuri yote waliyokuwa wakifanya wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani na kuzingatia mafundisho waliyopewa hata baada ya mfungo huo.

Katika kukabiliana na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa jamii, Shehe Mavumbi amewataka waislamu na wasio waislamu kujiepusha na vitendo vyovyote vilivyo kinyume na maadili ambavyo havimpendezi Mwenyezi Mungu.

Aidha ameungana na Mheshimiwa Rais kwa kuitaka jamii kuchukua tahadhari za mafuriko katika maeneo yao hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zimeendelea kunyesha kwa wingi katika Mikoa mbalimbali.

Akitoa salamu katika Baraza hilo Askofu Elias Mbagata wa Kanisa la Injili Afrika amempongeza Shehe Mavumbi na Mashehe wote wa BAKWATA kwa ushirikiano wao mzuri na Viongozi wa Madhehebu ya Kikristo Mkoani humo.

Amesisitiza kuwa Viongozi wa dini wana nafasi kubwa sana ya kuunganisha jamii na kuepusha vitendo vya uvunjifu wa amani, hivyo akaomba ushirikiano huo uendelee daima.