December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bajeti ya RUWASA Wilaya ya Kilindi 2024/2025 kuongeza upatikanaji maji

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Kilindi

WAKALA wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga imetangaza
mpango bajeti wa utekelezaji wa miradi ya maji kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa zaidi ya bilioni 3.2.

Ambapo kati ya fedha hizo zaidi ya bilioni 1 ni kutoka Serikali Kuu huku zaidi ya bilioni 2.1 ni fedha za wafadhili.

Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kilindi walipofika kukagua tenki la Mradi wa Maji Lwande uliopo Kata ya Lwande.

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa fedha hizo na kuweza kuongeza upatikanaji wa maji kwenye vijiji vya wilaya hiyo ni ile inayoendelea pamoja na miradi mipya ikiwa ni utafutaji wa vyanzo, uandaaji/usanifu wa miradi.

Hayo yamesemwa Februari 19, 2024 na Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Abdallah Isulla akisoma taarifa kwa niaba ya Meneja wa RUWASA Wilaya hiyo Mhandisi Alex Odena kwenye kikao cha Baraza la Bajeti la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Amesema Wilaya hiyo inategemea kuendelea na ukamilishaji wa miradi ya maji inayoendelea kujengwa kupitia fedha za Mfuko wa Maji yenye thamani ya bilioni 37.6.

“Mradi wa Maji Kwamaligwa/Gitu ya bilioni 6.9,mradi wa maji Diburuma/Songe ya bilioni 22.9,mradi wa maji Kilindi Asili ya bilioni 1.5,Bokwa/Mafulila zaidi ya milioni 765.2,ujenzi wa Bwawa la maji Saunyi (Lombout) bilioni 3.3,uchimbaji wa visima 23 katika vijiji 23 bilioni 1.5,ukamilishaji wa mradi wa maji Mabalanga milioni 465.5,” amesema.

Mhandisi Isulla amesema, Wilaya ya Kilindi inategemea kuendelea kutekeleza miradi mipya ya maji kupitia fedha za Mfuko wa Maji (NWF/GoT) yenye thamani ya bilioni 13.5.

Ambayo ni ujenzi wa Bwawa la maji Msente bilioni 2.3,mradi wa maji Kwaluguru/Negero bilioni 6.3,
ujenzi wa mradi wa aji Nkama milioni 949.1na ujenzi wa Bwawa la maji Mnkonde ya bilioni 2.6.

Wataalamu wa RUWASA Wilaya ya Kilindi wakiwa kwenye moja ya kituo cha maji (kilula) Mradi wa Maji Jungu/Balang’a.

Pia amesema, Wilaya ya Kilindi inategemea kuendelea kutekeleza miradi ya maji (inayoendelea) kupitia fedha za wafadhili (PforR) yenye thamani ya milioni 739.1,ambayo ni
ukarabati/upanuzi mradi wa maji Mgera/Kisangasa zaidi ya milioni 306.3,
ujenzi wa mradi wa maji Kwaluguru/Negero milioni 400.6 na
ukarabati wa mradi wa maji Chamtui zaidi ya milioni 62.1.

Sanjari na hayo Wilaya hiyo inategemea kuendelea kutekeleza miradi ya maji (miradi mipya) kupitia fedha za wafadhili (PforR) yenye thamani ya bilioni 1.7.

Miradi hiyo ni ujenzi wa mradi wa maji Ludewa milioni 368.6,upanuzi wa mradi wa maji Kilindi Asili/Misufini milioni 379.6,ujenzi wa mradi wa maji Mkindi milioni 941.4 na kuboresha huduma ya maji katika shule nne (4) za sekondari ya milioni 66.3.

Aidha amesema mamlaka hiyo kwa Kilindi ina jumla ya skimu za maji 42, mtandao wa mabomba ya vipenyo tofauti yenye umbali wa mita 238,352, matanki ya kuhifadhia maji 81 ya ujazo tofauti wa kati ya lita 1,000 hadi 450,000, vituo vya kuchotea maji 694 vyenye jumla ya koki (water taps) 1,011 zinazofanya kazi.

“Miundombinu hii inatoa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 140,294 sawa na asilimia 39.1 ya wakazi 398,391 wa Kilindi na mkakati uliopo ni kufikia asilimia 85,” amesema Mhandisi Isulla.

Tenki la ujazo wa lita 75,000 katika Kijiji cha Mafulila, Kata ya Kikunde.

Vilevile amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024, RUWASA Wilaya ya Kilindi hadi kufikia Februari 2024
imepokea zaidi ya milioni 961 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya lipa kwa matokeo (PforR) na zaidi ya milioni 354 za utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF).

Hivyo kufanya jumla ya fedha zilizopokelewa katika bajeti ya 2023/2024 kuwa ni bilioni 1.3 sawa na asilimia 39.51 ya bajeti yao ambayo ni bilioni 3.3.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Bajeti 2024/2025.