March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bahati Ndingo:Wananchi washuhudia kazi kubwa ya Rais Samia,Mbarali

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline, Mbarali

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya,kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM)Bahati Ndingo, amesema hana shaka na wananchi wa jimbo hilo kwa kuwa ndani ya kipindi kifupi wameona kazi kubwa iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, licha ya changamoto kadhaa ikiwemo za barabara.

Akizungumza kuhusu vipaumbele vyake kwa wananchi, Ndingo amesema ataendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara, elimu, afya na upatikanaji wa maji safi.

“Kwenye ilani ya uchaguzi ya kila mkoa, tumeona jinsi tulivyopewa kipaumbele, hususan kwenye barabara ambazo zimekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Mbarali. Vilevile, changamoto ya maji imeanza kupatiwa suluhisho kupitia jitihada kubwa za serikali kuhakikisha maeneo yote yanapata huduma hiyo.

Aidha Ndingo amesema serikali imeendelea kusogeza huduma za afya kwa kujenga vituo vya afya katika kata mbalimbali.

Ameeleza kuwa zaidi ya kata 12 ,tayari zina vituo vya afya, huku kata nane zikiwa bado hazijapata huduma hiyo, lakini kupitia ilani ya CCM, mipango ya ujenzi wa vituo vipya tayari imewekwa.

Kuhusu sekta ya elimu, Ndingo amesema katika ilani ya uchaguzi imeainishwa mikakati ya ukarabati wa shule kongwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.

Ameongeza kuwa sekta ya kilimo nayo imepata mageuzi makubwa kupitia miradi ya umwagiliaji na uchimbaji wa mabwawa, hatua zinazolenga kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija.

“Ni wazi kuwa Wilaya ya Mbarali imekuwa kinara wa kilimo, na kupitia miradi hii mikubwa tunaamini nguvu za wakulima wetu zitazidi kuimarika. Kwa msingi huo, sina shaka na dhamira njema ya Rais Samia, kwani tumeshuhudia maendeleo makubwa tangu alipoingia madarakani”amesema Ndingo.

Tutawaeleza wananchi kazi za miaka minne iliyopita ambazo zinaendelea kwa vitendo,” aliongeza Mgombea huyo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali, Maranyingi Matukuta, amesema wananchi wa Mbarali wana imani kubwa na chama hicho kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa chini ya usimamizi wa Rais Samia.

“Yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika awamu ya sita, ikiwemo fedha nyingi zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Mheshimiwa Bahati Ndingo amekuwa sehemu ya utekelezaji huo, na tunaamini kwa kushirikiana na baraza la madiwani atapewa tena ridhaa na wananchi,”amesema Matukuta.