April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bahati Nasibu ya Taifa, Vodacom zashirikiana kurahisisha miamala kidijitali

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

BAHATI Nasibu ya Taifa, imesaini ushirikiano na Kampuni ya Vodaco, Ili kurahisisha miamala ya bahati nasibu ya Taifa na kupanua fursa za kibiashara kupitia mfumo wa fedha wa kidijitali.

Kuunganishwa kwa bahati nasibu ya Taifa kwenye jukwaa la M-Pesa, kutawapa watumiaji urahisi wa upatikanaji wa michezo ya bahati nasibu kupitia jukwaa salama.

Kwa kutumia mtandao mpana wa Vodacom wenye zaidi ya watumiaji milioni 26, ushirikiano huu utawezesha urahisi wa ununuzi wa tiketi za michezo ya kubahatisha, kupitia majukwaa ya kidijitali ya Vodacom, ikiwemo huduma za M-pesa kwa njia ya simu, USSD codes na aplikesheni ya M-pesa.

Mkurugenzi wa ITHUBA Tanzania, Kelvin Koka (kulia) na Meneja Biashara wa M-pesa, Kelvin Nyanda (kushoto) wakitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kupanua wigo wa Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania nzima kupitia jukwaa la M-pesa.

Akizungumzia hilo Mkurugenzi wa ITHUBA Tanzania, Kelvin Koka amesema ushirikiano huo ni hatua kubwa katika sekta ya michezo ya kubahatisha nchini.

“Ushirikiano huu na M-Pesa utahakikisha kwamba wachezaji wanashiriki kikamilifu katika michezo ya bahati nasibu, huku ukihamasisha wafanyabishara kuweza kushirikiana nasi kwa kuwa jukwaa letu linazingatia uwazi na mustakabali ujao wa bahati nasibu ya Taifa.

“Kwa kuwa M-Pesa ni mshirika wetu rasmi wa huduma za kifedha kwa njia ya simu, tutahakikisha kwamba tunazingatia usalama, ufanisi na uhakika wa miamala ya wateja wetu,” amesema Koka.

Mkuu wa Idara ya wa M-pesa Tanzania, Jacqueline Ikwabe alibainisha umuhimu wa ushirikiano huu kwa kusema, “M-Pesa imejikita katika kuwezesha uvumbuzi wa kidijitali unaowanufaisha wafanyabiashara na wateja.

“Kwa kuiunganisha Bahati Nasibu ya Taifa kwenye jukwaa letu, tutahakikisha ushiriki salama, wa haraka na rahisi huku tukifungua fursa zaidi za ushirikiano katika sekta mbalimbali.”

Bahati Nasibu ya Taifa inalenga kutumia ushirikiano huo kuongeza uelewa wa huduma zake na kuimarisha uaminifu kabla ya uzinduzi rasmi wa Bahati nasibu ya Taifa.

Hatua hiyo inatarajiwa kuweka msingi wa ushirikiano katika sekta ya michezo ya kubahatisha na fedha nchini Tanzania.

Ujumuishwaji wa jukwaa la Bahati nasibu ya Taifa kwenye majukwaa ya Vodacom Tanzania utarahisisha ununuzi wa tiketi na upatikanaji wa maudhui ya michezo ya kubahatisha kwa Watanzania wengi zaidi hapa nchini.

Hatua hiyo ya kimkakati inatarajiwa kuongeza ushiriki wa umma, kupanua wigo wa huduma na kuhakikisha ushiriki mpana kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu.