Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
BAHATI Nasibu ya Taifa , imetangaza ushirikiano wa kimkakati na Shirika la Posta Tanzania, kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa michezo ya kubahatisha inapatikana kwenye jukwaa hilo.
Kupitia ushirikiano huo, huduma ya Bahati Nasibu ya Taifa itapatikana katika ofisi 207 za Posta, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa michezo ya kubahatisha kwa Watanzania, mijini na vijijini.
Mtandao mpana wa Shirika la Posta, wenye jumla ya ofisi 430 zinazohudumia wastani wa watu 79,140 kwa kila kituo, utatoa jukwaa thabiti kwa Bahati Nasibu ya Taifa kufanikisha dhamira yake ya kuwafikia Watanzania wote.

Kwa kuunganisha huduma za bahati nasibu katika vituo hivi, ushirikiano huu utahakikisha kuwa hata jamii zilizo maeneo ya mbali zinapata fursa ya kushiriki katika michezo ya kubahatisha.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Mkurugenzi wa ITHUBA Tanzania, Kelvin Koka amesema ushirikiano na Shirika la Posta Tanzania ni hatua kubwa katika kuhakikisha ujumuishi wa Watanzania wote kwenye michezo ya kubahatisha.
“Kupitia mtandao mpana na wa kuaminika wa Shirika la Posta, tutafanikisha azma yetu ya kuwafikia wananchi wote na kuwapa nafasi ya kushiriki kwa urahisi. Huu ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kusaidia maendeleo ya taifa kupitia michezo ya kubahatisha,” amasema Koka.

Kwa upande wake, kurugenzi wa Biashara za Kielektroniki na Huduma za Kifedha wa Shirika la Posta Tanzania, Constantine John Kasese amesema Shirika hilo limejikita katika kuwaunganisha wananchi na huduma muhimu kote nchini.
“Ushirikiano wetu na Bahati Nasibu ya Taifa ni sehemu ya jitihada zetu za kutoa huduma bunifu zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu.
“Kuwepo kwa michezo ya bahati nasibu katika ofisi zetu kutaleta urahisi kwa wananchi kupata tiketi za michezo ya kubahatisha na kuchangia juhudi za maendeleo ya jamii,” amesema Kasese.
Kwa kutumia miundombinu madhubuti ya Shirika la Posta Tanzania, Bahati Nasibu ya Taifa inalenga kutoa michezo ya kubahatisha inayozingatia urahisi, usalama, na uwazi kwa washiriki wote, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuboresha maisha ya Watanzania.

More Stories
Team nane kuchuana ” Bwigane Tv Ramadhan Street Cup”
Nkya ameibuka bingwa ,michuano ya Lina PG Tour
Bahati Nasibu ya Taifa, Mixx by Yas kushirikiana kimkakati