January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya mazao uharibika kwa kukosa wanunuzi Rungwe

Na Esther Macha, Timesmajira, Online,Mbeya 

HALMASHAURI ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imewaomba wawekezaji wa kuongeza thamani ya mazao kujitokeza kuwekeza katika halmashauri yao ili kuokoa uharibifu wa mazao ya kilimo na mifugo ambayo huwa yanaharibika kutokana na kukosa wanunuzi.

Akizungumza kwenye maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Rungwe, Juma Mzara amesema wilaya hiyo inajihusisha na kilimo cha mazao ya aina mbalimbali na wanazalisha kwa kiwango cha juu pamoja na ufugaji.

“Tunahitaji wawekezaji wengi zaidi ili tuweze kuipaisha Rungwe kwani sisi ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula,kilimo na maziwa ,kwa kuwa msimu wa Kilimo huwa tunazalisha kwa wingi mpaka kuharibika kutokana na kukosa wawezekezaji na hata mboga mboga na matunda huharibika pia,”amesema.

Aidha Mzara amesema kuwa kwa wilaya ya Rungwe wanazalisha lita za maziwa mil.54 kwa mwaka pamoja na kwamba wana mwekezaji mmoja Asasi ambaye ununua maziwa lakini bado hatoshi.

Mmoja wa wakulima Zadiel Mapunda amesema kuwa baadhi ya wanufaika waliowezeshwa kupitia vyama vya ushirika na mikopo ya halmashauri wameishukuru serikali na kuiomba iendelee kupunguza bei za dawa na vifaa vinavyotumika kwenye mifugo.

“Hii itasaidia kuendelea kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa wakulima ambao wanajishughulisha na kilimo katika maeneo mbalimbali yaliyopo wilayani Rungwe”amesema mkulima huyo.

Rashid Mwakosya ni mfugaji kutoka halmashauri ya Wilaya ya Rungwe amesema wamefurahishwa kuona hamasa kubwa kwa wakulima na wanashukuru kuletwa kwenye maonesho hayo ambayo lengo ni kujifunza.