Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MASHIRIKA baadhi yasiyo ya kiserikali (NGO’s) na vituo vya kulelea watoto yatima yanadaiwa kujinufaisha kwa fedha za misaada inayotolewa na wahisani kusaidia watoto hao.
Madai hayo yametolewa na Mkuu wa Idara ya Falsafa na Maadili,Chuo Kikuu cha Mtakafifu Agostino (SAUT) Mwanza,Padri Dkt.Innocent Sanga,wakati wa chakula na watoto yatima kilichotolewa na BAKWATA mkoani humo ilishirikiana na Rocky Solution Ltd.
Akizungumza kabla ya chakula hicho Padri Dkt.Sanga amesema baadhi ya NGO’s na vituo vya kulelea yatima vinawatumia watoto hao kibiashara na kujinufaisha kwa fedha za misaada inayotolewa na wahisani.
Amesema serikali katika kukomesha tabia hiyo itunge sera ya kuvipata vituo vya kuwalea,kuwatetea na kuwalinda yatima pamoja na kutengeneza mifumo ya kuwabaini katika vitongoji,vijiji na mitaa.
“Tahadhari,serikali yawezekana inaogopa, baadhi ya NGO’s na vituo vya watoto yatima vinawatumia kibiashara na kujinufaisha,wanawafanya kama bidhaa na wanakula fedha zao baada ya kuandika maandiko ya kuomba fedha kwa wahisani,”amesema Padri Sanga.
Ameishauri serikali kuhakikisha vituo na mashirika hayo yanasajiliwa,ufanye uratibu na ufuatiliaji kwa wanaojinufaisha kwa fedha za yatima na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Tumewakandamiza yatima kwa njia mbalimbali,Tanzania imegeuka janga kubwa la yatima kudhulumiwa,kuonewa na kunyang’anywa mali zao na ndugu,hivyo tutafakari dhambi hii na kutubu,”amesema Padri Dky.Sanga.
Mkuu huyo wa Idara ya Falsafa na Maadili ya chuo cha SAUT Mwanza,pia ameishauri serikali itenge bajeti ya kuwasaidia yatima kupata elimu na miongoni mwao wana uwezo mkubwa kiakili.
Pia amesema changamoto ya watoto yatima kukimbilia mitaani ni matunda ya kutukanwa na kukandamizwa na ndugu zao ili kuwaepuka maadui hao wanaowakamindamiza wakihofia usalama wao.
Aidha Padri Dr.Sanga amesema mila za kigeni zimeharibu upendo kwani mila za kiafrika kukaa na yatima ni kawaida na kumhudumia kama familia ni utamaduni wetu,hivyo huwezi kumwacha akakimbilia mtaani kwani dini zetu zinashughulika na mema kwa matendo na si maneno.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Wakili Kiomoni Kibamba,katika chakula hicho amesema kujiona tuko katika dunia ya ustaarabu kumesababisha kuacha misingi kwa kukosa ucha Mungu.
“Zamani miji yote haikuwa na watoto wa mitaani,tujiulize wametoka wapi?,tunazidi kuharibikiwa na kuiharibu jamii,bila kujali imani tumebaki na majina ya dini na kukosa ucha Mungu,tumekuwa dhulumati na roho mbaya,”amesema.
Wakili Kibamba amesema hakuna mcha Mungu ataadhirika na anayetaka kufanikiwa amchukue yatima na kumlea kwani hakutaka kufiwa na wazazi na Mungu alivyo fundi kifo hakichagui cheo, kabila, rangi wala kabila ya mtu.
Awali Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke amesema anatamani kuona kila Mtanzania akimchukua yatima na kuishi naye na kutoa wito kwa waliojaliwa kuwa na uwezo kiuchumi wavisaidie vituo vinavyowalea yatima.
“Mtume Muhammad S.A.W.anasema atakayekaa na yatima na kumtendea vizuri atakuwa naye bega kwa bega,natamani kila Mtanzania amchukue yatima na kumtendea wema ili kumuondolea huzuni aliyo nayo,”amesema.
Pia ameeleza kuwa chakula hicho cha pamoja na yatima huandaliwa kila mwaka na kampuni ya The Rocky Solution kwa miaka sita sasa.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza