Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI wa Maji, Jumaa Awesso amesema,Wizara ya Maji ilikuwa wizara ya kero na lawama kutokana na ufinyu wa bajeti, changamoto ambayo imetatuliwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza fedha hadi shilingi Trilioni 3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini ambayo imekuwa ikiendelea kutekeleza miradi 878 vijijini na miradi 200 katika maeneo ya mjini.
Awesso amesema hayo jijini hapa leo Januari 28,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi ya siku 100 za Rais Samia katika kipindi chake cha pili ambapo amesema katika kutekeleza azma yake ya kumtua mama ndoo kichwani

Katika kipindi cha miaka minne pekee ya uongozi wake, Rais Samia amefanikiwa kufikisha maji katika vijiji 7,929, jambo ambalo ni rekodi ya kipekee.
“Tangu Rais Samia aanzishe kauli mbiu kumtua mama ndoo kichwani changamoto za ukosefu wa maji kwa wananchi zimepungua kwa kiasi kikubwa na zilizopo ni chache ambazo tutahakikisha tunazimaliza na kuhakikisha vijijini vyote vilivyobaki vimepata maji,”Amesisitiza

Hata hivyo Waziri huyo amesema kuwa Wizara yake imejipanga kikamilifu kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza, huku akiahidi kuwa watumishi wa wizara hiyo hawatakuwa kikwazo katika kufikia lengo hilo.
“Rais wetu ni mama, na anajua adha wanayopata akina mama kutokana na ukosefu wa maji. Hataki kusikia wala kuona akina mama wa nchi hii wakiteseka kufuata huduma hiyo muhimu,”amesema Awesso.
Waziri huyo amebainisha kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya maji vikiwemo maziwa makuu kama Victoria, Tanganyika na Nyasa, pamoja na mito mikubwa kama Ruvuma, Pangani, Rufiji na Malagarasi. Alisema wizara itatumia rasilimali hizo kikamilifu ili kuhakikisha maji yanawafikia wananchi popote walipo.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina