June 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso:Rais Samia ameweza kumtua mwanamke ndoo kichwani

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Pangani

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amesema kwa kiasi kikubwa, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanikiwa kumtua mwanamke ndoo kichwani baada ya kufikisha huduma ya maji kwenye vijiji 10,800 kati ya vijiji 12,318.

Ameyasema hayo Juni 14, 2025 kwenye uwekaji wa Jiwe la Msingi ujenzi wa upanuzi Mradi wa Maji Mikocheni kwenda Kijiji cha Mkwaja, Kata ya Mkwaja, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga. Jiwe la Msingi liliwekwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi.

“Mkuu wa Wilaya ya Pangani Gift Msuya akizungumza kwenye Mradi wa Maji Mikocheni.”

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameapa kumtua mwanamama ndoo kichwani. Nchi yetu ya Tanzania ina vijiji 12,318, mpaka sasa ameshafika vijiji 10,800, tumebakisha vijiji 1,500. Kwa kasi hii ambayo wanaifanya RUWASA, na mitambo 25 tumepewa kila mkoa (mtambo mmoja kila mkoa), nataka niseme, hakuna kijiji cha nchi hii kitakosa huduma ya maji safi na salama, sababu Rais Dkt. Samia amejipanga,  na ndiyo suluhu ya kutatua matatizo ya maji” amesema Aweso.

Aweso amesema amehudumu kwenye Wizara ya Maji kwa miaka minane, akianza na Naibu Waziri wa Maji miaka mitatu, na Waziri wa Maji miaka mitano. Huko nyuma, Wizara ya Maji ilikuwa ya kero na lawama, na hata bajeti zake zilikuwa zinapita bungeni kwa mbinde.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi, Mkuu wa Wilaya ya Pangani Gift Msuya (kushoto) na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Pangani Rajabu Yahya (kulia) wakikagua Mradi wa Maji Mikocheni.”

“Mimi nimepata wasaa  wa kuwa Waziri kwenye Wizara ya Maji kwa miaka nane sasa. Wizara yetu miaka ya nyuma ilikuwa wizara ya kero na lawama, na bajeti za Wizara bungeni ilikuwa ni mtihani kupita. Ukipita kwa wananchi, nao wananchi wanalalamika juu ya adha ya maji.

“Dkt. Samia alipopata nafasi ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Maji aliipa maelekezo mafupi ya kwamba yeye ni mama, na wanaoteseka na adha ya maji ni akina mama. Hataki kusikia wala kuona akina mama wa nchi hii wakiteseka na adha ya maji. Kunakusema na kutenda, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anasema na kutenda, na leo tunaona matendo yake hapa Mkwaja” amesema Aweso.

“Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi akiweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Mikocheni.”

Aweso amesema wananchi wa Mkwaja walikuwa wanatumia visima vya asili kuchota maji, huku maji hayo yakiwa hayatoshelezi mahitaji yao, lakini Rais Dkt. Samia amekwenda kuwatatulia kero ya maji baada ya kuwajengea mradi wa maji wenye thamani ya sh. 836,220,420, ambao unakwenda kuwaondolea kutafuta maji kwa kubahatisha.

“Amekwenda kutatua adha ya maji kwa wananchi wa Mkwaja. Wananchi wa Mkwaja kihistoria walikuwa wanatumia maji ya visima vya asili, lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia sh. milioni 836,220,420 kwa ajili ya mradi huu, haijawahi kutokea… wema unalipwa kwa wema” amesema Aweso.

Ussi amekiri, tangu ameanza kukimbiza Mwenge wa Uhuru Aprili 2, mwaka huu ameona utekelezaji mkubwa wa miundombinu ya maji, na kupongeza utendaji wa Aweso kwenye kumsaidia Rais Dkt. Samia kumaliza kero ya maji kwa wananchi nchini.

Ussi aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ili iwe endelevu, kwani pamoja na kujengwa kwa ajili ya kuweza kuwasaidia wao kupata maji kwa muda mrefu, pia miradi hiyo imejengwa kwa fedha nyingi.

“Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Pangani Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Kata ya Mkwaja.”

Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Pangani Mhandisi Rajabu Yahya, amesema ujenzi wa upanuzi Mradi wa Maji Mikocheni kwenda katika Kijiji cha Mkwaja uliopo kata ya Mkwaja unatekelezwa na Mkandarasi M/s Kharton Traders Ltd wa Dar es Salaam kwa Mkataba NA.AE-102/2021-2022/TAG/W/47 wenye thamani ya sh. 836,220,420 pamoja na VAT. Mkataba wa ujenzi wa mradi huo ulisainiwa  Agosti 24, 2022 na Mkandarasi kukabidhiwa eneo la mradi Septemba 8, 2022, ambapo utekelezaji wake ulikuwa wa miezi sita.

“Kutokana na changamoto ya kupata maeneo kwa wakati kwa ajili ya ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji pamoja na jengo kwa ajili ya Ofisi ya Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO), shughuli za ujenzi wa mradi huu zilichelewa kuanza. Aidha, kutokana na sababu zingine zilizojitokeza wakati wa utekelezaji mradi huu, unategemewa kukamilika Juni 30, 2025, ambapo hadi sasa mradi umetekelezwa kwa asilimia 80, na umeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi.

“Lengo la mradi huu ni kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wapatao 2,081 waishio katika Kijiji cha Mkwaja kupitia vituo vya kuchotea maji 13 (DPs) vilivyokwisha jengwa pamoja na maunganisho ya maji majumbani. Ujenzi wa mradi huu unatekelezwa kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF na PforR), ambapo hadi sasa Mkandarasi amelipwa jumla ya sh. 438,240,802 kupitia hati ya malipo Na. 1 na Na.2” amesema Mhandisi.

“Waziri wa Maji Jumaa Aweso (wa nne kulia), Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (wa tano kulia), na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani Beatrice Kasimbazi (wa tatu kulia) wakiwa kwenye kuwekwa Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Mikocheni.”

Mhandisi Yahya amesema kazi zilizotekelezwa hadi sasa kwa mujibu wa mkataba ni, ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita 90,000 katika mnara wa mita sita, ujenzi wa Ofisi ya Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) upo katika hatua ya ukamilishwaji, ujenzi wa bomba kuu (raising main) na bomba za kusambazia maji (Distribution network) mita 8,176, ujenzi wa vituo 13 vya kuchotea maji na ujenzi wa uzio katika tenki.

“Kazi ambazo hazijakamilika ni, kupeleka umeme wa TANESCO kwenye jengo la Ofisi ya CBWSO, Ukamilishaji wa jengo la Ofisi ya CBWSO, ujenzi wa uzio katika Ofisi ya CBWSO, ukamilishaji wa vyoo katika Ofisi ya CBWSO, ujenzi wa valvu chemba 14 na uwekaji wa alama 107 (Marker post) juu ya njia za bomba.

“Ofisi ya RUWASA Wilaya ya Pangani kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Mkwaja, inatoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa mradi huu ambao utawapunguzia wanajamii wa kijiji cha Mkwaja adha ya kutumia muda mrefu wa   kutafuta maji badala ya kutumia muda huo kwenye shughuli za kiuchumi” amesema Mhandisi Yahya.

“Tenki la maji lita 90,000 kwa ajili ya wananchi wa Mkwaja.”