Na Yusuph Mussa, Timesmajira Pangani
WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ametaka fedha za miradi ya maji zisiliwe mbichi badala yake ziwekwe kwenye akaunti benki na zitolewe kwa utaratibu kwa ajili ya kuhudumia miradi hiyo ili iwe endekevu.
Amesema miradi ya maji inatakiwa iwe endelevu ndio maana kumeundwa Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) kwa ajili ya kusimamia miradi ili iwe endelevu na kufanya kazi ndogo ndogo ya kuitunza.
Ameyasema hayo Aprili 16, 2024 wakati Mwenge wa Uhuru ulipo zindua mradi wa maji Kwakibuyu ambapo ameeleza kuwa kula fedha mbichi kunaleta mfarakano kwenye kamati, kwani leo Mwenyekiti akichukua pesa na mmoja wa wajumbe, kesho wengine watataka wapewe, hivyo kamati inavunjika.
“Huu ni mradi mkubwa ambao utatahakikisha wananchi wanapata maji kwenye nyumba zao na hiyo ni dhamira njema ya Rais wetu Dkt. Samia,miradi hii inatumia fedha nyingi, hivyo niwaombe kuilinda na kuitunza kama mboni ya jicho,”ameeleza na kuongeza kuwa
“Tumeweka mfumo mzuri kuwa fedha zinapokusanywa ni lazima zikawekwe kwenye akaunti ya benki sio ule mfumo leo anapewa Mwenyekiti anamgawia mjumbe fulani, mwingine kanyimwa ugomvi na kamati inavunjika, hilo hatuwezi kukubali,”.
Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani,amewataka wananchi wa Kijiji cha Kwakibuyu, Kata ya Kipumbwi kuulinda mradi huo ili uwe endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza na wananchi hao kabla ya kuzindua mradi huo Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava amesema mradi huo ni muhimu kwa jamii kwa vile unakwenda kuwanufaisha wananchi 5,868.
Akisoma taarifa ya mradi huo wa maji Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Pangani Mhandisi Rajab Yahya amesema mradi unatekelezwa na Mkandarasi M/S Matrix Technology Company Ltd wa Dar es Salaam kwa Mkataba Na. AE -102/2021-2022/TAG/W/43 wenye thamani milioni 594.2 pamoja na VAT.
“Mkataba wa ujenzi wa mradi ulisainiwa Desemba 30, 2021 na Mkandarasi kukabidhiwa eneo la ujenzi
Januari 7, 2022, ambapo mkataba ulikuwa wa kipindi cha miezi sita,kutokana na sababu za kupata maeneo ya ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji, jengo la kufunga mitambo ya pampu
pamoja na jengo la ofisi ya Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) kutopatikana kwa wakati, shughuli za ujenzi wa mradi huu zilichelewa kuanza,”.
Pia ameeleza kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na unatoa huduma ya maji ambao umelenga kutoa huduma masaa 24 ambapo bei ya maji ni sh. 1,400 kwa unit moja (sawa na lita 1,000).
Huku lengo likiwa
ni kutoa huduma ya maji safi na salama katika maunganisho nyumbani kwa wananchi 5,868 sawa na kaya 1,467 katika Kijiji cha Kwakibuyu, ambapo hadi sasa maunganisho ya watu 1,720
sawa na kaya 430 yamefanyika ambapo CBWSO ya MIKI inaendelea kuwafanyia maunganisho kaya ambazo bado.
Mhandiai Yahya amesema ujenzi wa mradi huo unatekelezwa kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF) ambapo hadi sasa Mkandarasi amelipwa 324,680,572, na kazi zilizotekelezwa na kukamilika katika mradi huo kwa mujibu wa Mkataba ni, ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 135,000 katika mnara wa mita sita.
Ujenzi wa jengo la kufungia mitambo ya kusukumia maji (Pump House), ujenzi wa bomba kuu (Rising main) na bomba za kusambazia maji
(Distribution network) mita 10,643, kufunga pump na vifaa vya nishati ya umeme, kujenga ofisi
ya chombo cha CBWSO, kupeleka umeme wa TANESCO (Three Phase) katika Pump House na ujenzi wa valvu chemba 14.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa