Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha kuwa uzalishaji wa maji kutoka Ruvu Juu, Ruvu Chini na Kigamboni unagawiwa kwa usawa katika maeneo yote yanayohudumiwa na mamlaka hiyo.
Aidha, ameitaka DAWASA kuweka ratiba wazi ya mgawanyo wa maji ili wananchi wa Tandale, Sinza na maeneo mengine waweze kujipanga kujua siku na muda wa kupata huduma hiyo.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, Waziri Aweso amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya maji, ambapo DAWASA ina uwezo wa kuzalisha lita milioni 534 kwa siku.
Hata hivyo, changamoto ya ukame kutokana na kuchelewa kwa mvua, hususan katika eneo la Ruvu Chini, imeathiri uzalishaji huo.Aweso amewaomba wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kuwa na mshikamano katika kipindi hiki cha mpito, akibainisha kuwa watabiri wa hali ya hewa wametoa taarifa za mvua kuanza kunyesha hivi karibuni.
Amesema Wizara imetoa maelekezo hayo ili kuhakikisha utoaji wa huduma unakuwa wa haki, na ameonya kuwa atafanya ufuatiliaji ili kujiridhisha kwamba DAWASA inalitekeleza kikamilifu kwa manufaa ya wananchi.
Waziri Aweso pia ametoa wito kwa wadau wa sekta binafsi wenye visima vikubwa au wanaotoa huduma za maji kushirikiana na Serikali katika kipindi hiki, akisisitiza kuwa changamoto hii haiwezi kubebwa na DAWASA pekee.
Aidha, ametaka visima vyote vilivyochimbwa na DAWASA na Wizara ndani ya Jiji la Dar es Salaam viunganishwe kwenye mfumo wa uzalishaji ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama, sambamba na kuzingatia ubora wa maji kwa ajili ya afya za wananchi.

Amehitimisha kwa kuwasisitiza wahariri na waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupaza sauti kuhusu umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema uzalishaji wa maji kwa sasa umepungua kutoka uzalishaji maji wa lita milioni 534.6 kwa siku hadi kufikia uzalishaji wa lita milioni 270 ambazo ni sawa na upufungu wa lita milioni 264.6 kwa siku.
Hata hivyo pamoja na upungufu huo imeeelzwa kwa hali ilivyosasa hivi sasa Mtambo wa Ruvu Chini iliyokuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 270 kwa siku hivi sasa unazalisha maji lita milioni 50 kwa siku huku Mtambo wa Ruvu Juu wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 196 ambapo sasa uzalishaji wake umepungua na kufikia lita milioni 150.
Aidha ametoa sababu za kupungua kwa uzalishaji maji na hivyo kusababisha changamoto ya uhaba wa maji katika mikoa ya Pwani ukiwemo Dar es Salaam.
Ametaja sababu za uhaba wa upatikanaji wa maji ni Mvua za masika zilinyesha chini ya wastani mwezi Machi – Mei, 2025“Kuchelewa kwa mua za Vuli zilizotarajiwa kunyesha kuanzia Oktoba – Desemba, 2025 na Mto Ruvu kuacha njia yake ya asili kwenye eneo la Kitomondo na kutengeneza mchepuko.“Sababu nyingine ni kuongezeka kwa Joto kutoka nyuzi joto 29-31C hadi nyuzi joto 33.2-34.2 (TMA), hali hii imepelekea kina cha maji kupungua kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo maji kupotea kwa njia ya Mvuke.
Ameongeza kuwa sababu nyingine ni kuongezeka kwa shughuli za kibanadamu (kilimo, ufugaji) ndani ya Bonde la Mto Ruvu.Bwire amesema DAWASA inawaomba wananchi kuwa wahimilivu katika kipindi hiki cha mpito na kuhifadhi maji yanayopatikana

“DAWASA na inaendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na upungufu wa maji kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanaendelea kupata huduma katika uwiano sawa.”Kuhusu hatua za muda mfupi zilizochukuliwa ni kusimamisha vibali vya watumia maji wengine ili kuruhusu DAWASA kupata maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Pia DAWASA kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Pwani, Bodi ya Bonde la Wami-Ruvu, inaendelea kufanya doria kwenye eneo la Mto Ruvu kuhakikisha hakuna matumizi mengine ya maji kutoka kwenye mto.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi