March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso apeleka neema Urambo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora

WAKAZI wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora wamelipuka kwa shangwe na furaha baada ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso kuagiza maji ya Ziwa Victoria yafikishwe wilayani humo ndani ya wiki tatu kuanzia sasa.

Aweso ametoa agizo hilo akizungumza na wakazi wa Wilaya hiyo katika Kata ya Muungano baada ya kutembelea na kukagua mradi wa maji wa Miji 28 unaotekelezwa na Serikali katika wilaya tatu za mkoa huo.

Amesema kuwa serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 143 ili kuleta maji ya uhakika ya Ziwa Victoria katika Wilaya za Kaliua, Urambo na Sikonge ambazo zinashida kubwa ya maji.

“Mradi huu utekelezaji wake unaenda vizuri,ujenzi wa tanki kubwa la kupokelea maji tayari limekamilika, na nimeambiwa kuwa kipande kilichobakia hakizidi hata kilometa moja maji yatakuwa yamefika hapa Urambo,” amesema Aweso na kuongeza:

“Nitawaongezea shilingi milioni 500 za mabomba ili kazi hii ifanyike haraka zaidi na maji yafike katika tanki ndani ya wiki tatu na kazi ya kuyasambaza kwa wananchi ianze mara moja,”.

Pia amesema ili kuhakikisha wakazi wa wilaya hiyo wanapata maji safi na salama ya uhakika aliahidi kuongeza kiasi cha shilingi milioni 400 ili RUWASA waweze kukamilisha haraka ujenzi wa mradi wa bwawa la maji la Kalemela.

Amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mwajuma Waziri,kuhakikisha fedha hizo zinaletwa haraka iwezekanavyo ili miradi hiyo miwili ikamilike kwa wakati na wananchi waanze kunufaika.

Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Hamis Mkanachi na Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta,wamesema furaha na shangwe ya wananchi itakamilika pale watakapoona maji hayo yamefika katika nyumba zao na kuanza kuyatumia,hivyo wamemuomba Waziri ambane Mkandarasi ili aharakishe kazi hiyo.