Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Miradi ya maji wilayani Misungwi,mkoani Mwanza ambayo utekelezaji wake umeonekana kusuasua wamchefua,Waziri wa Maji Jumaa Aweso,na kuamua kumuondoa kwenye nafasi yake, Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA),Wilaya ya Misungwi Mhandisi Marwa Kisibo,kutokana na kushindwa kusimamia utekelezaji wa miradi wilayani humo.
“Mtakuja kutugombanisha viongozi na watu,nimefuatilia utendaji wako wa kazi,hapa tutaleta mtu anayeweza kufanya kazi.Mbunge tutaweka mtu ambaye atatusaidia ili mambo yaweze kwenda,mfanye kazi mtu atakaye taka kufanya kazi tutampa ushirikiano,hauwezi kufanya kazi tutakuacha tu, kwani katika kila kazi kuna faida,maneno matupu uleta hasara,”amesisitiza Aweso.
Aweso, ametoa kauli hiyo Septemba 8,2024, alipotembelea na kukagua mradi wa chanzo cha maji Ukiriguru,ambao utekelezaji wake ulionekana kusuasua unaosimamiwa na RUWASA.
“Nilifika mpaka kwenye chanzo cha maji Ukiriguru,kuangalia utekelezaji wa mradi wa maji,kuna mambo ambayo nimeyagundua moja ni uzembe.Sisi tulipokea maelekezo mahususi ya Rais Samia,alisema yeye ni mama,na asilimia kubwa wanaoteseka juu ya adha ya maji ni wanawake.Akaeleza kuwa hataki kusikia wala kuona,wa mama wa nchi hii,wanateseka na adha ya maji na akaenda mbali zaidi akaniambia, Waziri wa Maji ukinizingua,nitanizingua,”amesema Aweso.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kata ya Usagara, wilayani Misungwi akiwemo Amina Ngusa, ameeleza kuwa wakazi wa maeneo hayo,wana changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji,ambayo wamekuwa wakiyatafuta kwa muda mrefu.
“Kila tukiomba maji hatupewi, naimani kwa ujio wa Waziri wa Maji,tunaweza tukapata maji tukatuliwa ndoo kichwani.Sisi wa mama tunahangaika mno, miaka mingi tunateseka,”ameeleza Amina na kuongeza:
“Wilaya ya Misungwi,miradi ya maji ni mingi,nafikiri wakandarasi wanakuwa ni wazembe wa kutekeleza kazi walizopangiwa.Serikali isiwafumbie macho,kwa mzembe,ambaye anashindwa kutimiza wajibu wake waondolewe,kwani kuna watu ambao wanaweza kufanya kazi na kutekeleza miradi kwa wakati na wakatusaidia sisi wananchi kupata huduma,”.
Ameeleza kuwa,maji wayafuata kwenye visima vijiji jirani,ambayo wananunua ndoo moja ya lita 20 kwa sh.300.
“Visima hivyo vilichimbwa na watu,ambapo tunatumia takribani masaa mawili kufuata maji hayo.Hali hiyo inachangia kurudisha uchumi na maendeleo nyuma, kwani muda ambao tungetumia kutafuta ridhiki kwa ajili ya watoto,tunatuamia kutafuta maji,”ameeleza Amina.
Naye Tunu Baluani, ameeleza kuwa hupatikanaji wa maji wilayani Misungwi,ni shida na tatizo.Na maji yanawafanya wananchi wa Usagara na Kata nyingine wilayani hapo kuwa na maisha magumu.
“Tunaona kuna miradi imeelekezwa huku kwetu,katika Wilaya hii,lakini utekelezaji wake ni wa kusuasua.Ambapo changamoto ni watendaji wamekuwa ni tatizo wa kukwamisha miradi,”ameeleza Baluani na kuongeza:
“Ninachoomba ni hatua kuchukuliwa kwa wazembe wote,hii habari ya kuwa tunaleana leana ina sababisha wananchi wanapata shida,wanaendelea kuteseka huku serikali ikiwa imeisha toa maelekezo na fedha.Sasa viongozi wanaohusika wachukue hatua stahiki dhidi ya watendaji wazembe ili wananchi wapate nafuu,”.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito