January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AUWSA kukausha majitaka yatokayo na kinyesi kuwa Mkaa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Arusha(AUWSA),imesema Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Shirika la SNV la Uholanzi imekamilisha ujenzi wa mtambo wa kutibu tope kinyesi katika eneo la Murieti,ambapo wameanza kukausha kinyesi hicho nakutengeneza mkaa.

Hayo yamesemwa jiji hapa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA,Mhandisi Justine Rujomba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka 2022/23 ambapo amesema lengo la kukausha kinyesi hicho kuwa mkaa ni kuweka jiji la Arusha katika hali ya usafi.

“Pia tumeangalia changamoto ya ukataji miti kwajili ya kuchoma mkaa ni kubwa kwa jiji la Arusha ndio maana tumeona kuna haja ya kufanya maji taka hayo kwa maana ya kinyesi kuwa mkaa na tumefikia asilimia  100 katika kuutengeneza lakini imetubidi tujiridhishe kwa maana ya ubora wa matumizi yake hivyo tumepeleka mkaa huo kwa wenzetu wa Shirika la viwango Tanznania (TBS)ili tusije tukatengeneza zaidi ukaleta madhara,”amesema.

Ameeleza kuwa Mtambo huo utasaidia kupokea na kuchakata majitaka yanayobebwa na magari ya majitaka kutoka sehemu mbalimbali za Jiji la Arusha.

“AUWSA imefanikiwa kuongeza mtandao majitaka (sewerage coverage) katika jiji la Arusha kutoka asilimia 8.03 mwaka 2020/21 hadi asilimia 24 mwaka 2021/22,

“Ili kuwafikia wananchi ambao bado hawajajiunga kwenye mtandao wa majitaka AUWSA kwa sasa inatoa huduma ya uondoaji majitaka kwa kutumia gari za majitaka ambapo Mamlaka inajumla ya gari tano za majitaka,Gari mbili za ujazo wa Lita 5,000 na gari tatu za ujazo wa lita 10,000,”amesema Mha.Rujomba.

Mkurugenzi wa AUWSA akiongea na Waandishi wa Habari ukumbi wa Habari Maelezo,Dodoma.

Akizungumzia vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 wa AUWSA,Mha.Rujomba amesema ili kuendelea kuboresha huduma na kufikia azma ya Serikali ya kuboresha huduma ya majisafi mijini kufikia asilimia 95,Mamlaka hiyo imeweka vipaumbele sita katika bajeti hiyo.

Ametaja kipaumbele kimoja wapo kuwa ni
Kukamilisha utekelezaji wa mradi mkubwa wenyewe gharama ya shilingi bilioni 6.5 ambao mkandarasi yupo katika kipindi cha uangalizi toka Julai 7 mwaka huu.

“Hii itakuongeza hali ya upatikanaji wa majisafi kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 100 ya wakazi wa Jiji la Arusha mwaka 2023,”amesema.

Pia ametaja Shughuli zitakazotekelezwa kuimarisha huduma ya Maji Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, ambapo amesema Mamlaka hiyo imepanga kutekeleza miradi inayogharimu shilingi bilioni 11.8 ya fedha za ndani za Mamlaka ili kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma katika eneo lake.

” AUWSA itajenga mtandao mpya wa majisafi kwa urefu wa kilomita 215.961 katika maeneo mbalimbali,itaunganisha wateja wapya 13,993 kati ya hao wateja 10,893 katika Jiji la Arusha, na wateja 3,100 miji midogo,kuongeza mtandao wa majitaka kwa kilomita 10 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha,Kuunganisha wateja 4,200 katika huduma ya uondoaji wa majitaka,”amesema.

Hata hivyo Mh.Rujomba amesema Mamlaka hiyo itajenga chemba za kuhifadhia dira za wateja dhidi ya uharibifu na wizi wa dira za maji, ambapo chemba 1,237 zinajengwa ili kuhamishia dira 5000 za wateja wa majumbani.

“Kumekua na changamoto ya wizi wa maji hadi sasa zaidi ya watu 55 wamekamatwa kwajili ya wizi wa maji na tukiwakamata tunakaa nao chini tunawaelekeza juu ya utunzaji miundombinu ya maji baada ya hapo wanalipa faini na hadi kufikia sasa waliokamatwa wamelipa faini ya shilingi milioni 65 za Tanzania,”amesema.

Pamoja na hayo amesema kuwa Mamlaka imeendelea kupanua huduma baada ya kuongezewa maeneo ya kutoa huduma ikiwamo kata saba za Wilaya ya Arumeru, pamoja na miji midogo ya Longido, Monduli, Ngaramtoni na Usa River.

“Mahitaji halisi ya maji kwa sasa ni lita milioni 124.7 kwa siku kwa mchanganuo ambapo Jiji la Arusha mahitaji  lita milioni  109.6 huku miji midogo mahitaji yakiwa lita milioni  15.09,”amesema.

Aidha amesema Maji yanayozalishwa kwasasa ni lita Milioni 84.5 kwa siku kutoka kwenye vyanzo vya visima virefu, chemchem na mito sawa na asilimia 68 ya mahitaji. huku matarajio ni kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini kulingana na lengo lililowekwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kabla ya kufika mwaka 2025.

“Kabla ya uwekezaji wa Serikali kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa, uzalishaji wa maji ulikua ni wastani wa lita Milioni  40 kwa siku na huduma ya uondoaji wa majitaka ilikua ni wastani wa asilimia 7.6 ya wakazi wa Jiji la Arusha ambapo kwa sasa kiwango cha uzalishaji maji kimeongezeka kwa lita Milioni 26 kwa siku,

“Ongezeko hilo limewezesha kuboresha upatikanaji wa maji kwenye maeneo yaliyokuwa na uhaba wa maji hasa katika maeneo ya Moshono, Kiserian, Murrieti, Olasiti, Sombetini, Kwa Moromboo, Olmoti, Sokoni 1, na baadhi ya maeneo ya Terati na kuchangia kuongeza saa za huduma kutoka masaa 15 hadi 19 kwa siku.