Judith Ferdinand,Mwanza
MKAZI mmoja wa kitongoji cha Buhaji Kijiji cha Igenge Kata ya Mbarika Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza, Anastazia Zakaria anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 40- 45, ameuwawa baada ya kupigwa na kitu kizito kichwani na mme wake.
Tukio hilo lililotokea Aprili 26 mwaka huu saa 4 usiku baada ya kushambuliwa na mume wake aitwaye Laurent Herman mwenye miaka kati ya 50-55 ambaye naye ni mkazi wa kitongoji cha Buhaji kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na kupelekea kufariki dunia papo hapa.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP Muliro Jumanne, amesema mara baada ya kufanya tukio hilo mwanaume huyo aliamua kunywa sumu ya madawa ya kilimo kwa lengo la kujiua, lakini majirani waliosikia kelele walifika nyumbani hapo na kumnywesha maziwa ili kunusuru uhai wake na baadae walitoa taarifa polisi.
ACP.Muliro amesema, jeshi hilo lilifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kushirikiana na wananchi kumpeleka mwanaume huyo kituo cha afya cha Mbarika lakini jana Aprili 27, mwaka huu saa moja na dakika 15 asubuhi alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Inadaiwa kuwa, chanzo cha mauaji hayo ni mwanaume huyo ambaye hakuwepo nyumbani kwake kwa kipindi kirefu kumuomba mkewe tendo la ndoa lakini mwanamke huyo alikataa akidai mpaka wakapime afya zao (UKIMWI) baada ya kuwa na mashaka na hali ya kiafya ya mume wake ndipo mwanaume huyo alikasirika na kupelekea ugomvi uliopelekea vifo vyao.
Miili ya marehemu wote wawili imehifadhiwa kituo Cha afya Mbarika kusubiri uchunguzi wa daktari na utakapokamilika itakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best